Home BUSINESS MCHECHU: MABADILIKO KWA TAASISI ZA UMMA NI SAFARI INAYOZINGATIA UFANISI NA MSHIKAMANO

MCHECHU: MABADILIKO KWA TAASISI ZA UMMA NI SAFARI INAYOZINGATIA UFANISI NA MSHIKAMANO

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, Akizungumza katika Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) unaofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere,  leo Februari 24, 2025, Kibaha, Pwani.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo, Hamad Abdallah, akizungumza na wajumbe Baraza la wafanyakazi, wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi kuzungumza katika mkutano huo.

PICHA NA HUGHES DUGILO 

Na; Mwanishi wetu, DAR ES SALAAM

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, amesema kuwa mageuzi katika taasisi za umma ni safari isiyoepukika, ikilenga kuimarisha utendaji, kuongeza ufanisi, na kupunguza utegemezi wa serikali katika uendeshaji wa mashirika yake.

Akizungumza katika Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) unaofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha, Mchechu amebainisha kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina imeanza kuchukua hatua za msingi kuhakikisha taasisi zinazojitegemea zinafanya mageuzi yenye tija.

“Reforms is a journey – mabadiliko ni safari, ni lazima tuyafanye kwa umakini na dhamira ya kweli,” amesema Mchechu, akifafanua kuwa mwaka huu serikali imeanza kutumia mfumo wa ukaguzi wa CAG katika kutathmini vigezo vya utendaji kazi (KPI). Amesema kuwa taasisi 58 zinazojitegemea zimeanza kupitia mchakato huu ili kuhakikisha zinajiendesha kwa weledi na uwazi.

Katika jitihada za kuimarisha uwajibikaji, Msajili wa Hazina amesema kuwa serikali itateua taasisi maalum kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa viashiria vya utendaji (KPI Monitoring) ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa na utegemezi unapunguzwa.

KUIMARISHA MATUMIZI YA RASILIMALI NA KUDUMISHA MSHIKAMANO

Mchechu ameweka wazi kuwa changamoto kubwa iliyopo ni jinsi ya kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi ili taasisi ziweze kujitegemea na kutoa huduma bora kwa wananchi. Ameeleza kuwa mafanikio ya mageuzi haya yanahitaji mshikamano na uwajibikaji wa pamoja kwa wafanyakazi wote.

“Ili tufanikiwe, tunahitaji kuwa na timu inayofanya kazi kwa upendo, siyo kwa majungu. Mimi mwenyewe ninaweza kuwa mmoja wa waathirika wa majungu, lakini nawaombeni sana mfanye kazi kwa upendo,” amesema Mchechu, akisisitiza kuwa uteuzi wa viongozi na watendaji hautazingatia maneno ya pembeni bali utazingatia ufanisi na uwezo wa mtu katika kutekeleza majukumu yake.

Ametoa wito kwa wafanyakazi wa taasisi zote za umma kushikamana na kushirikiana kwa karibu katika mchakato wa mageuzi, kwani mshikamano ndiyo msingi wa mafanikio.

“Hatutateua mtu kwa sababu ni bingwa wa kupiga majungu, tutateua kwa ufanisi. Naomba tuwe na mshikamano ili kuhakikisha taasisi zetu zinapiga hatua kubwa katika maendeleo,” amesisitiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHC ambaye pia, ni Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo, Hamad Abdallah amempongeza Msajili wa Hazina kwa misingi mizuri aliyoiweka wakati akiongoza Shirika hilo, nakwamba kwa sasa Shirika limeweza kuongeza mapato yake ambapo ankara za kodi ya nyumba zimepanda kutoka shilingi 7.5 bilioni mwaka 2021 hadi kufikia shilingi 9.4 bilioni,ambapo makusanyo ya kodi hiyo yamefikia zaidi ya asilimia 100.

Aidha, amesema kuwa thamani ya Shirika kwa mwaka 2024 imekuwa na kufikia Shilingi 5.04 trillioni, na Shirika limeendelea kupata faida huku likiendelea kulipa kodi za Serikali ambazo ni wastani wa Bilioni 30 kwa mwaka.

Ameoneza kuwa hatua hiyo limelifanya Shirika kwenda kuandika historia kwa kutoa Gawio la Serikali, ambapo kwa mwaka huu Shirika litatoa Gawio la Shilingi Bilioni 6.5, nakwamba tayari nusu ya fedha hizo zimeshalipwa.

Mkutano huo wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NHC umeendelea kwa mijadala yenye lengo la kuimarisha utendaji wa shirika, kuboresha huduma kwa wananchi, na kuhakikisha mageuzi yanatekelezwa kwa tija na uwazi.