Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe. Eunju Ahn, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 19 Februari 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe. Eunju Ahn mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 19 Februari 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe. Eunju Ahn mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 19 Februari 2025.
DODOMA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe. Eunju Ahn, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 19 Februari 2025.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema Tanzania inathamini na imedhamiria kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Korea ulioanza tangu mwaka 1992 ambao unachagiza maendeleo katika sekta mbalimbali nchini. Ameipongeza Jamhuri ya Korea kwa kuiunga mkono Tanzania katika sekta ya Elimu, Miundombinu, TEHAMA, Afya, Kilimo, Viwanda na Nishati.
Amesema makubaliano ya ushirikiano baina ya Tanzania na Korea katika madini ya kimkakati yataleta manufaa mengi zaidi kwa kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na madini mengi ambayo yanaenda sambamba na mwelekeo wa dunia ya sasa ambayo inajikita katika uchumi wa teknolojia za kijani.
Aidha Makamu wa Rais amemueleza Balozi wa Jamhuri ya Korea umuhimu wa kuongeza kiwango cha ufanyaji biashara baina ya Tanzania na Korea yenye manufaa kwa pande zote mbili. Amesema ni muhimu wawekezaji na wafanyabiashara wa Korea kutembelea Tanzania mara kwa mara ili kujionea fursa zilizopo na kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda. Amesema uongezaji wa thamani kwa malighafi hapa hapa nchini utachochea biashara, uhamishaji teknolojia pamoja ongezeko la ajira kwa wananchi wa Tanzania.
Pia Makamu wa Rais amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Jamhuri ya Korea katika kubadilishana wafanyakazi, ambapo amemsihi Balozi huyo kuwezesha mchakato wa kujiunga katika Mfumo wa Vibali vya Ajira (EPS) ili wafanyakazi wa Tanzania waweze kuingia katika soko la ajira la Korea na kufanya kazi katika sekta mbalimbali kama vile ujenzi wa meli, sekta ya viwanda na kilimo cha kisasa.
Halikadhalika amesema ushirikiano unahitajika katika Elimu na kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya kwa kuwapatia mafunzo katika ubingwa na ubobezi wa utoaji matibabu mbalimbali. Makamu wa Rais pia amesisitiza kushirikiana katika masuala ya utamaduni, michezo na lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe. Eunju Ahn amesema katika kipindi atakachohudumu nafasi ya Ubalozi nchini Tanzania, atahakikisha anasimamia na kuharakisha kukamilika kwa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa baina ya Tanzania na Jamhuri ya Korea ikiwemo ushirikiano katika madini ya kimkakati na maendeleo ya uchumi wa buluu.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
19 Februari 2025 – Ikulu – Chamwino