Na Dk. Reubeni Lumbagala
Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni chama kikongwe nchini Tanzania, kikiwa kimetimiza miaka 48 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977. Ukongwe wa chama hiki hauonekani tu katika umri wake, bali pia katika uzoefu wake wa kisiasa, uongozi imara, na utekelezaji wa sera zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Kwa kuwa lengo kuu la chama chochote cha siasa ni kushika dola, CCM inaonekana kuwa na dhamira thabiti ya kuendelea kuongoza kwa kuhakikisha inasuka kikosi chake vyema kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliofanyika jijini Dodoma Januari 18-19, 2025, wajumbe kwa sauti moja walimpitisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia chama hicho.
Kazi kubwa na nzuri zilizofanywa na serikali inayoongozwa na CCM Bara na Zanzibar, hususan utekelezaji wa Ilani ya 2020-2025, zimekuwa sababu ya msingi za kuwapendekeza viongozi hawa waendelee kuongoza ili kukamilisha programu zao mbalimbali za maendeleo. Wananchi ni mashuhuda wa miradi mikubwa ya kimkakati inayogusa maisha yao moja kwa moja, jambo linalothibitisha kuwa viongozi hawa wanastahili kuendelea na majukumu yao.
Kwa muktadha huu, vitendo vina sauti kubwa kuliko maneno. Katika kampeni zijazo, Dk. Samia na Dk. Mwinyi watakuwa na kazi rahisi ya kuonyesha mafanikio yao na kuwasilisha mipango mipya itakayojumuishwa katika Ilani ya 2025-2030.
Dk. Nchimbi: Kiungo Muhimu katika Kikosi cha Ushindi
Katika mkakati wa kusuka kikosi bora zaidi, Mkutano Mkuu Maalumu ulimuidhinisha Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuwa mgombea mwenza wa Rais Dk. Samia katika uchaguzi wa Oktoba 2025.
Dk. Nchimbi ni mwanasiasa mwenye sifa za kipekee na uzoefu wa hali ya juu ndani ya chama na serikali. Amehudumu kama Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mkuu wa Wilaya, Mbunge, Naibu Waziri, Waziri kamili, Balozi wa Tanzania nchini Brazil na Misri, na sasa Katibu Mkuu wa CCM. Ni mzalendo, mchapakazi, na mwanasiasa shupavu ambaye kambi ya upinzani inaweza kuwa haina mtu wa kufanana naye kwa sifa na weledi.
Stephen Wasira: Nguli wa Siasa na Nguzo ya Chama
Mkutano Mkuu Maalumu pia ulimchagua kwa kishindo mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira, kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) kufuatia kujiuzulu kwa Abdulrahman Kinana mwaka jana.
Wasira ni mwanasiasa mahiri mwenye uzoefu mkubwa katika chama na serikali. Ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya TANU na CCM, ikiwa ni pamoja na kuwa Mkuu wa Mkoa, Mbunge, Naibu Waziri, na Waziri kamili. Baada ya kuchaguliwa, alisisitiza kuwa kazi kuu ya CCM ni kushinda uchaguzi na kushika dola, akieleza kuwa maandalizi ya ushindi wa 2025 yameanza tangu uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024.
Kwa umahiri wake wa kujenga hoja, Wasira anabaki kuwa silaha muhimu ya CCM katika siasa za ushindani, hasa dhidi ya wapinzani ambao mara nyingi hutegemea mihemuko badala ya hoja na sera mbadala.
Kwa kikosi hiki chenye viongozi waadilifu, wachapakazi, na wenye uzoefu wa hali ya juu, hakuna shaka kuwa CCM inaenda kwenye uchaguzi ikiwa imara zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Kwa miaka mingi, chama kimekuwa na utaratibu wa kuchagua wagombea wanaokubalika na wananchi, jambo linalorahisisha ushindi wake. Baada ya kuthibitishwa kwa viongozi wa juu wa chama, hatua inayofuata ni uteuzi wa wagombea wa ubunge na udiwani ambao pia watapaswa kuwa wenye sifa na kukubalika kwa wananchi.
Timu ya CCM ya 2025 ni imara, yenye rekodi ya mafanikio, na inayotoa ushindani wa hali ya juu. Kwa upande mwingine, vyama vya upinzani bado vinaonekana kulemewa na malalamiko dhidi ya katiba na tume ya uchaguzi badala ya kuwasilisha sera mbadala zinazoweza kuwashawishi wananchi.
Ndiyo maana nasema, kwa CCM hii yenye kikosi imara kutoka juu hadi chini, inaishindaje eeh! Unaishindaje? Muda utaongea, lakini tayari salamu zimeshatumwa kupitia ushindi wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana.
Maoni: 0620 800462