![](https://greenwavesmedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/MG_7801-1.jpg)
DAR ES SALAAM
Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!JUKWAA la Asasi za Kiraia za Ukanda wa Maziwa Makuu limetoa wito kwa vikundi vya waasi Mashariki mwa DRC Congo kusitisha mapigano ambayo yamesababisha vifo kwa wananchi wasio na hatia.
Wito huo ni moja ya maazimio ya Jukwaa hilo lililokutana Jijini Dar es Salaam kwa siku mbili, ambapo pamoja na mambo mengine wameunga mkono maazimio ya Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) waliokutana februari 8,2025 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Akisoma maazimio hayo Mjumbe wa Jukwaa la Asasi za Kiraia Nchi za Maziwa Makuu, Kennedy Walusala kutoka nchini Kenya, amesema wamekutana kwa siku mbili Dar es Salaam kupitia uratibu wa Jukwaa la Kitaifa la Asasi za Kiraia la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Kanda wa nchi za Maziwa Makuu, Mzee Joseph Butiku.
![](https://greenwavesmedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/MG_7817.jpg)
![](https://greenwavesmedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/MG_7761.jpg)
Walusala amesema asasi za kiraia, zilizokutana Jijini humo, Februari 7 hadi 9, mwaka huu, zinaunga mkono maamuzi ya mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi za EAC na SADC nakwamba hali ya ukosefu wa usalama nchini Congo sio nzuri na hatua kali zinahitajika kuchukuliwa haraka.
Amesema iwapo mgogoro huo hautashughulikiwa kwa dharura, kuna hatari ya hali kuwa mbaya zaidi na kuhatarisha utulivu wa kanda nzima.
Mjumbe huyo amesema kuna haja ya kuongeza juhudi za pamoja kudai suluhisho la kudumu na shirikishi.
Amesema kwamba maazimio hayo ni pamoja na kusitishwa kwa mapigano mara moja na kuondolewa kwa vikosi vya kigeni vilivyoingia katika ardhi ya DRC bila mwaliko.
Amesema asasi hizo, zinaunga mkono azimio la kurudisha amani DRC, kupatikana kwa haki kwa waathiriwa wa machafuko hayo.
“Pia tunaunga mkono uamuzi wa kuunganisha michakato ya Luanda na Nairobi, ili kuwezesha mazungumzo kati ya DRC na Rwanda, huku wakisisitiza umuhimu wa kusitisha mapigano mara moja na kwa ufanisi,” amesema.
Walusalo amesema kwamba, washiriki wamesisitiza umuhimu wa mtazamo wa pamoja wa kanda, ili kuhakikisha kwamba kuna mwitikio wa pamoja na wa kina kuhusu changamoto za kiusalama, kibinadamu, na kisiasa zinazoikumba DRC na Kanda ya Maziwa Makuu kwa ujumla.
Aidha, amesema asasi za kiraia katika Ukanda wa Maziwa Makuu zitatoa ushirikiano wa kila aina pale ambapo utahitajika ili kuhakikisha wananchi wa DRC wanakuwa na amani yakudumu.
![](https://greenwavesmedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/MG_7765.jpg)
![](https://greenwavesmedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/MG_7844.jpg)
![](https://greenwavesmedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/MG_7751-Copy.jpg)