Home LOCAL JAJI WARIOBA: NAPONGEZA CCM KWA HATUA ZAKE DHIDI YA RUSHWA

JAJI WARIOBA: NAPONGEZA CCM KWA HATUA ZAKE DHIDI YA RUSHWA

Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, amepongeza hatua zilizoanza kuchukuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mapambano dhidi ya rushwa kwenye uchaguzi.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Jaji Warioba ametoa pongezi hizo akirejea mabadiliko ya Katiba ya CCM yaliyofanywa na Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, yakiwemo marekebisho ya namna ya kupata wagombea wa udiwani, uwakilishi na ubunge, kwa kuongeza idadi ya wapiga kura wa vikao vya kura za maoni.

Amesema kwa kuwa vita dhidi ya rushwa si ya siku moja, CCM haina budi kuhakikisha mapambano ya kumshinda adui huyo yanakuwa endelevu kwa kusimamia misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho.

Mhe. Warioba, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Mstaafu, amesema hayo katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, leo Alhamisi, tarehe 20 Februari 2025, baada ya Balozi Nchimbi kumtembelea nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kumjulia hali.

Aidha, Jaji Warioba, mbali na kukumbusha kuhusu misingi ya CCM, alisisitiza sifa na miiko ya uongozi ilivyoainishwa kwenye Katiba ya CCM, akisema chama kina wajibu wa kuendelea kuwapatia matumaini Watanzania kwa kutoa uongozi bora kwa mwelekeo sahihi wa nchi.

“Hivi mlivyoanza ni safi, in the long run (hatimaye huko mbele) tutakuwa na mwanga wa mapambano dhidi ya rushwa. Nilikuwa very interested (na hamu kubwa) kujua mabadiliko hayo kwenye Katiba ya Chama, nilivyoshindwa kuwepo kwenye Mkutano Mkuu Maalum. Ni muhimu sana CCM iendelee kusimamia misingi yake, ikiwemo ahadi za mwanachama.

“Vita hii si ya siku moja, ni muhimu muda wote chama kitafute njia za kuzuia rushwa kwa kusimamia misingi yake. Watu wazungumzie sifa na miiko ya uongozi. Wazungumzie sera, si hela. Kihistoria, CCM ni chama cha itikadi, sera na ilani. Kina wajibu wa kuonesha matumaini wapi tunawapeleka watu,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:

“Hivi mlivyoanza kupambana na rushwa itasaidia… mmeanza… naomba tu msikate tamaa. Jingine muhimu ni hili suala la kutoa mafunzo, pia ni muhimu sana. Wanachama na viongozi ni muhimu wakijue chama vizuri, hadi huko chini kabisa kwa wananchi. CCM ni tofauti na vyama vingine. Tunao wajibu wa kufanya kwa watu.”

Aidha, alisema vyama vya siasa nchini vinapaswa kutofautiana kwa sera na dira ya namna ya kuwatumikia watu, badala ya kutumia muda mwingi kuzungumzia namna ya kupata madaraka.

Jaji Warioba alisisitiza pia umuhimu wa CCM kuendeleza na kuimarisha utamaduni wake wa kupokea mawazo mapya ili kujiimarisha zaidi katika maisha na hali ya watu, huku kikitumia utaratibu wake wa miaka mingi katika kuandaa viongozi bora kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania

Katika hatua nyingine, Mjane wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere, ameitaka CCM kuendelea kutimiza wajibu wake wa kuzisimamia serikali zake zote mbili ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uwezo wa kujitegemea, hasa katika kujilisha.

Mama Maria alisema hayo alipokutana na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, aliyefika nyumbani kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Msasani, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kumsabahi na kumjulia hali, leo Alhamisi, tarehe 20 Februari 2025.

“Naomba tu muendelee kusimamia sera ya msingi ya CCM kuhusu kujitegemea… Uhuru wa taifa unakamilika zaidi pale taifa linapojitegemea, hasa katika kujilisha na kuwa na chakula. CCM isiache wajibu wake wa kuzisimamia serikali zake zote mbili ili nchi yetu iendelee kujitegemea,” alisema Mama Maria.