Home LOCAL DAWA ZA KIFAFA KUPATIKANA KATIKA VITUO VYOTE VYA KUTOLEA HUDUMA AFYA.

DAWA ZA KIFAFA KUPATIKANA KATIKA VITUO VYOTE VYA KUTOLEA HUDUMA AFYA.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kutoa huduma na dawa kwa wagonjwa wa kifafa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini, ili kuhakikisha kila mgonjwa anapata matibabu stahiki.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Mhe. Aida Joseph Khenani, aliyetaka kujua kama Serikali haioni haja kwa sasa kutoa huduma na dawa kwa wagonjwa wa Kifafa, amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, takribani wagonjwa 199,324 walipatiwa matibabu ya kifafa nchini, hatua inayodhihirisha jitihada za Serikali katika kuboresha huduma kwa wagonjwa wa magonjwa sugu.

Kwa mujibu wa muongozo wa matibabu wa kitaifa (Standard Treatment Guideline – STG), kuna aina nane (8) za dawa za msingi kwa matibabu ya kifafa zinazopatikana katika vituo vya afya kuanzia ngazi ya msingi, kulingana na hali ya mgonjwa.

“Serikali imeweka mfumo wa kuhakikisha dawa za kifafa zinapatikana kwa uhakika katika vituo vyote vya afya, kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007,” amesema Dkt. Mollel.

Serikali pia imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa wagonjwa wa kifafa kwa kuongeza upatikanaji wa dawa na kuboresha utoaji wa matibabu, hatua inayolenga kupunguza athari za ugonjwa huo kwa jamii.