
JESHI la Polisi mkoani Pwani, linamshikilia Tanganyika Masele (32), Mkazi wa Kisengile, Kitongoji cha Buduge, Kata ya Marui ,Wilayani Kisarawe, kwa kosa la mauaji ya mke wake (27) pamoja na mtoto mdogo, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Salim Morcase, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo, tukio lililotokea Februari 17, majira ya mchana, katika maeneo ya Kitongoji cha Buduge.
Morcase alieleza marehemu, aliyejulikana kwa jina la Gumba Kulwa, pamoja na mtoto wake, walifariki kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni, kisha miili yao kutupwa pembeni ya bwawa la maji lililopo karibu na nyumbani kwao.
Kamanda huyo alifafanua kwamba, uchunguzi wa awali umebaini kuwa Tanganyika Masele, mume wa marehemu Gumba Kulwa, alikuwa mara kwa mara akiahidi kumuua mkewe na mtoto wake.
“Mara baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani Pwani lilifika eneo la tukio na kufanya msako kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali ya Kijiji na wananchi, hatimaye kumkamata mtuhumiwa huyo,” alieleza Morcase.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano, na kwamba baada ya kukamilika kwa upepelezi, jalada la kesi litafikishwa ofisi ya mashtaka kwa hatua zaidi.
Kamanda Morcase alitoa wito kwa jamii kufuata sheria za nchi na kuacha tabia za kujichukulia sheria mkononi, hali inayosababisha madhara makubwa kwa wengine.