Home LOCAL WANANCHI TANGA WABARIKI MAAMUZI YA MKUTANO MKUU WA CCM TAIFA

WANANCHI TANGA WABARIKI MAAMUZI YA MKUTANO MKUU WA CCM TAIFA

 Na: Mwandishi Wetu, Tanga
Wananchi wa Tanga wamebariki kwa asilimia 100 azimio la Mkutano Mkuu wa CCM Taifa lililompitisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya Urais kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Hayo yameelezwa na  Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini (CCM) Ummy Mwalimu kwa niaba ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Januari 28, 2025 katika viwanja vya Community Centre jijini Tanga. Ummy amesema maamuzi ya Mkutano Mkuu ni sahihi kutokana na kazi nzuri na kubwa zilizofanywa na Rais Dk. Samia na Dk. Hussein Mwinyi huku wakitekeleza ipasavyo ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 katika kutatua kero za wananchi na kukuza maendeleo nchini.
“Ndugu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, ndugu zangu wa Tanga, naweza kusema ninayo mamlaka ya kusema kwamba, sisi wananchi wa Tanga Mjini ambao ndiyo wapigakura tunapongeza na kuunga mkono maamuzi ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa wa kumpitisha Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka 2025. Pia tunaunga mkono maamuzi ya kumpitisha Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea Urais Kwa upande wa Zanzibar na ndugu yetu, shemeji yetu Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu,”amesisitiza Ummy Mwalimu.
Sanjari na hilo, Ummy Mwalimu amesema kazi zilizofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan zinaonekana kwa macho na ndiyo maana katika mkutano huo makundi yote ya watu kama vile bodaboda, wavuvi, wajane, vijana, madereva wa magari wamehudhuria mkutano huo.
Katika hatua nyingine, Ummy Mwalimu amesema CCM ina mtaji wa kura za wananchi kwa sababu katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana, CCM ilipata ushindi wa asilimia 100 ambapo mitaa yote 181 ya Tanga Mjini inaongozwa na wenyeviti wa mitaa watokanao na CCM. Aidha, kazi nzuri zilizofanyika Tanga Mjini hasa katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, umeme, utoaji mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum, ni dhahiri CCM itapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu.
Mkutano huo pia umetumika kuzindua rasmi maandalizi ya maadhimisho ya miaka 48 tangu kuzaliwa CCM ambapo viongozi mbalimbali wa chama na serikali ngazi ya mkoa na wilaya wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Ustadhi Rajab Abdurahmani, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dk. Batilda Buriani na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Meja Hamisi Mkoba na wengine walipata fursa ya kuhutubia huku msisitizo mkubwa ukiwa ni kazi nzuri zilizofanywa na CCM katika kuwahudumia wananchi wake na kusukuma agenda ya maendeleo kwa ustawi wa wananchi.