Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mheshimiwa Hakainde Hichilema, amewasili jijini Dar es Salaam kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, unaofanyika nchini kuanzia tarehe 27 hadi 28 Januari 2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mheshimiwa Rais Hichilema alipokelewa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) pamoja na maafisa wengine waandamizi wa serikali.
Mkutano huo wa siku mbili umeanza tarehe 27 Januari 2025 katika ngazi ya Mawaziri, na tarehe 28 Januari 2025 Wakuu wa Nchi wataungana kujadili masuala muhimu kuhusu nishati barani Afrika.
Mkutano huu unawaleta pamoja Wakuu wa Nchi za Afrika, wadau wa sekta ya nishati, na washirika wa maendeleo kujadili mikakati ya kukabiliana na changamoto za nishati na kuchangamkia fursa za bara hili. Moja ya matokeo makubwa ya mkutano huu ni kupitishwa kwa Azimio la Dar es Salaam, linalosisitiza dhamira ya viongozi wa Afrika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu, na endelevu kwa maendeleo ya bara la Afrika.