MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Chama Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira, akizungumza na viongozi pamoja na wanaCCM waliojitokeza kumpokea katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM leo Januari 23, 2025 Jijini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Chama Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira, akinyanyua Mkuki juu mara baada ya kusimikwa kuma chifu wa kabila la wagogo na kupewa jina la MARUGU (Mpambanaji)
– Atoa maagizo kwa wizara kuchukua hatua
– Asisitiza CCM ni kimbilio la wanyonge
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Chama Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira, ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuhakikisha ardhi ya vijiji iliyoporwa kinyume cha sheria, inarudishwa kwa wananchi.
Wasira alitoa maagizo hayo Leo Januari 23, 2025 jijini Dodoma, wakati akizungumza na viongozi pamoja na wanaCCM waliojitokeza kumpokea katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM.
Alisema Sheria ya Ardhi ya Vijiji inazuia ardhi kuwa bidhaa ya kununua na kuuza kwa sababu ukiruhusu hali hiyo, kuna watu watakosa hata sehemu za kulala.
“Wapo watu wajanja, sheria ile inasema ukitaka ardhi ya kijiji zaidi ya ekari 25 lazima wanakijiji wakutane waandike muhtasari waseme tumekubali.
“Lakini hata wakiandika lazima uende halmashauri ya wilaya, kwa Waziri wa Ardhi na faili lifike kwa Rais kisha asaini. Kuna watu wamechukua ardhi huko vijijini na hawana saini ya Rais.
“Tunaiomba Wizara ya Ardhi, ikague ardhi ya kijiji iliyoporwa kinyume cha sheria, irudi kwa wanakijiji. Tatizo la rushwa duniani ndiyo hiyo unahalalisha kwa rushwa, unaweka majina hadi ya watu waliokufa ili ionekane ni halali,” alieleza.
Wassira alisema ukiuza ardhi wapo wenye uwezo wa kununua, hivyo wale wasio na uwezo kununua watakosa hata sehemu ya kukanyaga.
“Tutakanyaga wapi kwenye ardhi ya watu. Ukitaka kujenga kibanda wanakuuliza wewe una shilingi ngapi ya kununua ardhi. Kwa hiyo wasionacho watakuwa hawana kitu na matumaini hawana,” alisisitiza.
Alisema CCM imejikita katika kuhakikisha inaboresha huduma za jamii ili maisha ya wananchi yaendelee kuwa bora kila siku.
“Sera ambazo ziko ndani ya CCM huwezi kuzikuta katika chama kingine. Vyama vingine kazi yao ni kushikana mashati na kupinga mambo mazuri yanayofanyika chini ya chama tawala,” alisema.
Aliongeza: “Tunaamini tutaendelea kushika dola kwasababu mambo yaliyofanyika chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni makubwa na yanatosha kuwashawishi wananchi wakaendelea kutupa imani ya kuongoza tena.”
Kwa mujibu wa Wassira, alisema Rais Dk. Samia amefanya mambo makubwa ambayo yanagusa maisha ya wananchi moja kwa moja ikiwemo ujenzi wa madarasa, vituo vya afya, barabara, maji na vifaa vya kutolea huduma za afya hadi katika zahanati.
GAVU AFUNGUKA
Kwa upande kwake, Katibu wa NEC, Siasa na Oganaizesheni, Issa Gavu, alisisitiza wanachama kuendelea kukilinda Chama kwa nguvu zote.
Alimpongeza Wassira kwa kuchaguliwa kwa zaidi ya asilimia 98 na wajumbe wa Mkutano Mkuu maalumu wa CCM, kushika nafasi hiyo.
“Nimuhakikishie kuwa tutaendelea kuhamasisha wanaCCM kufuata maadili ya Chama ili tukupunguzie kazi za kufanya. Tutakupa ushirikiano wa kutosha utimize malengo na mikakati ndani ya Chama,” alisema.
Alisisitiza: “Hatuna shaka na utendaji kazi wako, wewe ni mtu muelewa, mnyenyekevu na mwenye msimamo. Tuna uhakika kwa kutumia uzoefu wako, CCM itapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu.”
KIMBISA AELEZA
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adamu Kimbisa, alisema hali ya kisiasa kwa mkoa huo ipo shwari kwani wanaendelea kujiandaa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Alisema Rais Dk. Samia amefanya kazi kubwa Dodoma, hivyo wananchi bado wana imani na CCM katika uchaguzi mkuu.
“Katika uchaguzi wa mwaka huu, tumejipanga kupata kura nyingi za CCM na hayo yote yanawezekana kwasababu ilani imetekelezwa ipasavyo katika maeneoo yote na wananchi wameona,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alimpongeza Rais Dk. Samia kwa kuaminiwa na Mkutano Mkuu kuwa kugombea Urais kupitia CCM katika uchaguzi wa mwaka huu.
“Kwa Mkoa wa Dodoma ilani ya CCM imetekelezwa na imepitiliza. Miradi mikubwa ya kimkakati inaendelea kutekelezwa na mingine imekamilika kwa asilimia kubwa,” alibainisha.