Kaimu Mkurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ofisi ya Zanzibar, Balozi Silima Kombo Haji, amesema ujio wa wajumbe wa mataifa mbalimbali unatoa fursa kubwa za utalii na uwekezaji nchini.
Akizungumza na Sheikh El Amin Omer El Amin kutoka Sudan aliyefika ofisini kwake Maisara kwa ajili ya kujitambulisha, Balozi Kombo alitumia fursa hiyo kumkaribisha kutembelea maeneo mbalimbali ya Zanzibar ili kujionea fursa za uwekezaji zilizopo kisiwani humo.
Balozi Kombo alieleza kuwa kwa sasa vipaumbele vya uwekezaji ndani ya Zanzibar ni pamoja na biashara ya utalii, viwanda, na uchumi wa buluu. Alimshauri Sheikh El Amin kufika Mamlaka ya Uwekezaji na Kukuza Uchumi Zanzibar (ZIPA) ili kupata maelezo ya kina kuhusu maeneo yaliyo tayari kwa uwekezaji.
Alifafanua kuwa uchumi wa buluu unajumuisha sekta muhimu kama vile uvuvi wa bahari kuu, utalii wa baharini kupitia visiwa vidogo vidogo, mafuta na gesi, pamoja na usafirishaji wa baharini. Aidha, Balozi Kombo alibainisha kuwa Watanzania na Wasudani ni ndugu wa muda mrefu, na uwekezaji wa Wasudani Zanzibar utazidi kuimarisha undugu huo.
Kwa upande wake, Sheikh El Amin Omer El Amin alisema ni mara yake ya kwanza kufika Zanzibar, na amevutiwa sana na nchi hiyo pamoja na ukarimu wa wananchi wake.