Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amefanya ziara katika mradi wa kihistoria wa Samia Housing Scheme unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Kawe, jijini Dar es Salaam. Ziara hiyo ililenga kukagua maendeleo ya mradi huo mkubwa unaolenga kuboresha makazi nchini.
Akiwa eneo la mradi, Mkuu wa Wilaya alipokea taarifa kutoka kwa Injiniya Grace Msita kuhusu hatua mbalimbali za utekelezaji. Mradi wa Samia Housing Scheme unalenga kujenga nyumba 5,000 kwa awamu, na umeendelea kwa kasi, ukiakisi dhamira ya NHC ya kuleta maendeleo kwenye sekta ya makazi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, kazi zilizopo sasa ni kufunga milango, kuimarisha mifumo ya lifti, na kupanga njia za watembea kwa miguu (pavement). Mradi huu unakadiriwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 48 hadi kukamilika kwake, ambapo tayari kiasi cha shilingi bilioni 30 kimelipwa kufanikisha kazi zilizokwishafanyika.
Imedokezwa pia kuwa iwapo mradi huu ungejengwa na mkandarasi wa nje, gharama zingefikia takriban shilingi bilioni 72. Hii ni ishara ya ubora wa NHC katika kufanikisha ujenzi wa nyumba bora kwa gharama nafuu.
Mkuu wa Wilaya amepongeza juhudi za NHC kwa kujenga nyumba zenye viwango vya juu kwa bei nafuu, huku akitoa wito wa kuendelea na kasi hiyo ili kuhakikisha azma ya kutoa makazi bora kwa Watanzania inatimia.
Mradi huu ni sehemu ya jitihada za kuimarisha makazi bora na ya kisasa kwa ajili ya Watanzania, na unaashiria ukuaji wa sekta ya ujenzi nchini.
#SamiaHousingScheme #MakaziBora #NHC #KwaMaendeleoYaMakazi