Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, ameonesha kuvutiwa na Mradi wa Samia Housing Scheme unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Kawe, jijini Dar es Salaam. Akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mtambule amepongeza juhudi za NHC za kubuni na kujenga makazi bora yanayopendezesha mazingira ya jiji na kuimarisha thamani ya mali za wilaya ya Kinondoni.
“Nimevutiwa sana na mradi huu. Ni mradi kielelezo kwa kuwa na nyumba nyingi, nzuri, na za kisasa ambazo zitadumu kwa muda mrefu huku zikipendezesha mazingira ya jiji letu la Dar es Salaam,” amesema Mtambule.
Amebainisha kuwa nyumba zote zilizojengwa kupitia mradi huo tayari zimeshanunuliwa, jambo linalodhihirisha mahitaji makubwa ya makazi bora. “Hili ni jambo la maana kwa wakazi wetu kupata makazi bora. Ninashauri mpate maeneo zaidi jijini Dar es Salaam ili muendelee kujenga nyumba bora kwani mnaboresha maisha ya wananchi na kusogeza huduma karibu,” aliongeza Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mtambule amepongeza mpango wa NHC wa kushirikisha sekta binafsi na ya umma katika kuboresha makazi na kuendeleza biashara. “Mpange vizuri upangaji wa makazi pamoja na biashara ili kuhakikisha kila mmoja ananufaika. Ushirikiano wenu na sekta binafsi ni jambo la kuigwa,” alisisitiza.
Mradi wa Samia Housing Scheme unaolenga kujenga nyumba 5,000 kwa awamu, unaendelea kwa kasi na ni sehemu ya jitihada za NHC za kuimarisha sekta ya makazi nchini.