Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam.
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imesema kwa kipekee kuwa mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati Safi, uliomalizika jana jijini Dar es Salaam, umekuwa wa mafanikio makubwa kwa sekta ya utalii na Taifa kwa ujumla kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akizungumza mara baada ya kuhitimishwa kwa mkutano huo, Afisa Masoko wa Bodi ya Utalii, Nassoro Hassan, alisema kuwa mkutano huo umetoa fursa muhimu kwa TTB kuwahamasisha wageni wa mkutano kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
“Kupitia mkutano huu, tumetumia teknolojia kuwasilisha taarifa muhimu kuhusu vivutio vya utalii nchini. Wageni walipata nafasi ya kuuliza maswali na kujifunza zaidi kuhusu namna wanavyoweza kutembelea vivutio hivyo,” alisema Hassan.
Hassan alibainisha kuwa mkutano huo ni hatua kubwa katika kuimarisha utalii wa mikutano na matukio (MICE tourism). Alisema mafanikio ya kuandaa mkutano wa kiwango cha kimataifa kama huo yanaimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha matukio makubwa yanayovutia wageni kutoka mataifa mbalimbali.
“Tanzania imeonyesha uwezo wa kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa, ambayo si tu inaleta wageni wengi nchini, bali pia inachangia kufungua fursa zaidi za kiuchumi na kiutalii,” alisema.
Hassan aliongeza kuwa nishati ni nguzo muhimu kwa sekta ya utalii na uhifadhi. Aliainisha kuwa matumizi ya umeme yameimarisha huduma za usiku katika hifadhi, pamoja na kuboresha huduma za hoteli na migahawa wanakopata huduma wageni.
“Nishati ina mchango mkubwa katika usalama wa hifadhi zetu usiku, matumizi ya majiko ya kisasa katika hoteli, na urahisi wa usafiri wa kitalii kupitia miundombinu kama treni ya mwendokasi ambayo imekuwa rahisi zaidi kwa watalii kufika Kusini mwa Tanzania,” alisema.
Hassan pia alieleza kuwa mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii yalikuwa kivutio kikubwa kwa wageni wa mkutano, ambapo walipata nafasi ya kujifunza kuhusu wanyama wakavu waliohifadhiwa, na kuhamasika kutembelea vivutio halisi.
“Kila mmoja aliyehudhuria maonesho ameona namna Tanzania ilivyopambwa kwa tunu zake za utalii, kuanzia wanyama hadi mandhari ya kuvutia. Wageni wengi wameonyesha nia ya kwenda kuviona vivutio hivyo kwa macho yao,” alisema.
Kwa kumalizia, Hassan alitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha miundombinu ya nishati, ambayo imekuwa kichocheo cha sekta ya utalii. Aliongeza kuwa Bodi ya Utalii Tanzania itaendelea kutumia mikutano kama hii kufungua fursa zaidi za kimataifa.
“Mkutano huu umekuwa wa mafanikio makubwa kwa Taifa. Tunaamini umefungua milango kwa matukio makubwa zaidi na wageni wengi zaidi kutembelea Tanzania,” alihitimisha Hassan.