Home LOCAL MAKAMU WA RAIS AFUNGUA KONGAMANO LA KISAYANSI LA MAJI

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA KONGAMANO LA KISAYANSI LA MAJI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Waziri wa Maji Jumaa Aweso wakati akiwasili katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam kufungua Kongamano la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji leo tarehe 29 Januari 2025.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishuhudia mtambo maalum wa kuchuja maji uliobuniwa na Chuo Cha Maji wakati akitembelea mabanda mbalimbali katika Kongamano la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji linalofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam. Tarehe 29 Januari 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua mabanda mbalimbali yaliyopo katika maonesho katika Kongamano la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji linalofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam. Tarehe 29 Januari 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji linalofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam. Tarehe 29 Januari 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa zawadi kutoka Chuo Cha Maji mara baada ya kufungua Kongamano la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji linalofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam. Tarehe 29 Januari 2025. ( Kushoto ni Waziri wa Maji Jumaa Aweso na kulia ni Mkuu wa Chuo cha Maji Dkt. Adam Karia)

DAR ES SALAAM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema tafiti zinahitajika zaidi katika menejimenti ya rasilimali maji ili kuwezesha maarifa mapya na uelewa mpana kuhusu upatikanaji na ubora wa maji

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji lililofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam. Amesema ni muhimu tafiti kuelekezwa kujibu changamoto zinazokabili menejimenti ya rasilimali za maji hususani kubaini, kuotesha na kutunza miti ya asili ambayo inafahamika katika maeneo mbalimbali ya kila wilaya au mikoa nchini kuwa ni rafiki wa maji.

Pia amesisitiza umuhimu wa tafiti hizo kuangazia teknolojia rahisi, endelevu na ya gharama nafuu ya kuvuna maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani, sambamba na uchimbaji wa mabwawa, na kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua yanayotiririka kwa ajili ya umwagiliaji wa mashamba na kukidhi mahitaji ya mifugo. Halikadhalika amehimiza umuhimu wa kuangazia tafiti  zitakazokuza  kilimo janja namna bora ya kurejesha  uasili wa maeneo yaliyoharibiwa na mmomonyoko wa udongo na ukame wa muda mrefu, kubuni mifumo, mbinu na hata motisha ya kutunza vyanzo vya maji na ardhi oevu pamoja na kuwianisha matumizi ya maji kwa binadamu, mifugo na wanyamapori.

Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwa Kongamano hilo kuangazia suala la kubuni mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama na huduma za uondoshaji majitaka kwa wote na kutoa kipaumbele kwa jamii zilizo katika mazingira hatarishi. Amesema suala hilo linapaswa kuhakikisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi yanajumuishwa katika mipango ya kila nchi ili kuendeleza matumizi bora ya maji na mifumo ya uondoaji wa majitaka pamoja na kujenga uwezo wa jamii kutambua, kuhimili na kukabiliana na matukio ya hali mbaya ya hewa.  

Hali kadhalika, Makamu wa Rais amesema majibu ya changamoto zinazohusu maji na uondoshaji wa majitaka ni jukumu linalohitaji nguvu ya pamoja ya wadau wote wa maji ndani na jumuiya ya kimataifa. Ameongeza kwamba kongamano hilo linapaswa kujadili namna ya kuhakikisha usalama na uendelevu wa rasilimali za maji, utupaji sahihi wa taka za sumu na hatarishi, kuweka mifumo endelevu ya kutenganisha aina mbalimbali za taka ngumu, matumizi ya maarifa asilia  katika menejimenti ya rasilimali maji kama vile upandaji wa miti asilia rafiki wa maji katika maeneo ya vyanzo vya maji na ardhi oevu.

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayo rahisisha ushirikiano katika uendelezaji wa rasilimali maji. Aidha amewaalika watafiti na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kushirikiana na Serikali katika menejimenti ya rasilimali maji.

Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema Chuo Cha Maji kimeendelea kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya maji nchini kupitia ufundishaji na uendelezaji wa wataalamu wa maji nchini pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu ikiwemo kufanya tafiti mbalimbali ili kuondoa changamoto zinazoikabili sekta hiyo. Amesema kongamano hilo ni sehemu ya kuimarisha upatikanaji wa mambo mapya  ikiwemo ubunifu na mbinu za kushughulikia changamoto za maji na usafi wa mazingira nchini. 

Awali Mkuu wa Chuo cha Maji Dkt. Adam Karia amesema kumalizika kwa kongamano hilo kutawezesha kupatikana kwa ripoti maalum itakayotumika katika matumizi mbalimbali ya sekta ya maji na mazingira. Amesema kutokana na umuhimu wa kongamano hilo, Chuo kimedhamiria kufanyika kwa kongamano hilo kila mwaka ili kujadili mambo muhimu na kupelekea uelewa wa pamoja katika masuala yote yanayohusua maji na usafi wa mazingira  

Kongamano hilo la siku tatu (29 – 31 Januari 2025) limeandaliwa na Chuo cha Maji, linawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya maji wa ndani na nje ya nchi ambalo lina kauli mbiu isemayo “Majibu ya changamoto za maji na uondoaji wa majitaka katikati ya mabadiliko ya tabianchi”. 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais 

29 Januari 2025 

Dar es Salaam.