NA MWANDISHI WETU KOROGWE
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete ameungana na ndugu, jamaa na marafiki katika mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Ernest Kimaya.
Mazishi ya Kimaya yamefanyika Januari 2, 2025 katika Kijiji cha Mnyuzi Wilaya ya Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.
Akizungumza wakati akitoa salamu za Serikali, Waziri Kikwete alimshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai wa Kimaya ambaye alianza harakati za kutetea watu wenye mahitaji maalum toka akiwa na miaka 19 miaka ya 1990.
Alisema Kimaya ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Taifa la Ushauri Kwa Watu Wenye Ulemavu amewahi kushiriki katika harakati mbalimbali atakumbukwa kwa kazi nzuri aliyoifanya akiwa Mbunge wa Bunge maalum, mabadiliko ya sera zinazosimamia ustawi wa wenye mahitaji maalum, na mafanikio mbalimbali.
Kwa upande mwengine Rais Dk Samia Suluhu Hassan alitoa shilingi milioni 3 kama rambirambi kwa familia ya Kimaya zilizopokelewa na mwanae Elizabeth Kimaya.
Marehemu Kimaya alifariki tarehe 30 Desemba, 2024 Jijini Dar es Salaam katika hospitali ya Ocean Road ambapo alikuwa akipatiwa matibabu.
Mwisho