Home Uncategorized BUNGE LAPITISHA MISWADA MIWILI YA MAREKEBISHO YA SHERIA

BUNGE LAPITISHA MISWADA MIWILI YA MAREKEBISHO YA SHERIA

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Miswada Miwili ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya 2024, leo tarehe 29, 2025 katika kikao cha pili cha Mkutano wa kumi nane  wa Bunge hilo.
Miswada iliyopitishwa leo ni pamoja na  Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mbalimbali (Na.3) wa Mwaka 2024 (The written Laws (Miscellaneous Amendments (No. 3) Bill 2024, na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2024 (The written Laws (Miscellaneous Amendments (No. 4) Bill 2024No. 3) Bill 2024.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha Miswada hiyo,  Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amesema kuwa  Miswada hiyo inakusudia kufanya marekebisho katika jumla ya Sheria kumi na mbili.
“Malengo ya marekebisho haya ni kuboresha utekelezaji wa masharti ya sheria husika na kuzifanya sheria hizi ziendane na wakati na kuleta tija kwa wananchi”. Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali 
Aidha, Mwanasheria Mkuu amezitaja Sheria zilizofanyiwa marekebisho ni Sheria ya Mawakili Sura ya 341, Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu Sura ya 3, Sheria ya Huduma za Jamii Sura ya 291, Sheria ya Shirika la Soko la Kariakoo Sura ya 132,  Sheria  ya Madini Sura ya 123 na Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298.
Mhe. Johari ameendelea  kuzitaja Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu Sura ya 423, Sheria ya Vyama vya Ushirika Sura ya 211, Sheria ya Tasnia ya Pamba Sura ya 201, Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji wa Kiuchumi Sura ya 386, Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji Sura ya 435, Sheria ya Ukaguzi wa Umma Sura ya 418.
Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema  marekebisho hayo yatasaidia kutatua changamoto na mapungufu mbalimbali yaliyokuwepo katika sheria hizo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge  ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Joseph Mhagama amefurahishwa na hatua za Bunge kupitisha Miswada hiyo ambayo inaenda kuleta maboresho katika utekelezaji wa Sheria zilizorekebishwa hivyo kupelekea mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii kwa watanzania.