Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!
NA MWANDISHI WETU
MKUTANO wa viongozi wa Umoja wa Afrika (AU), utakaofanyika mwezi Februari mwaka huu, pamoja na ajenda nyingine unatarajiwa kupitisha rasmi Azimio la Nishati (MISSION 300), ambalo liliridhiwa na viongozi walioshiriki Mkutano wa Viongozi hao jijini Dar es Salaam kuanzia Januari 28 hadi 28 mwaka huu.
Hayo yameelezwa leo katika taarifa ya Benki ya Dunia Group (WBG) ambapo imeweka jana hadi sasa benki hiyo na wadau wengine wamechanga zaidi ya dola za Marekani bilioni 50 kwa ajili ya utekelezaji MISSION 300.
“Mwezi ujao Februari AU ina kikao cha nchi wanachama, hivyo watatumia fursa hiyo kupitia azimio hilo la MISSION 300 rasmi,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliendelea kusema kiwa Wakuu wa Nchi na Serikali 30 za Afrika wamejitolea kwa mageuzi na hatua madhubuti za kupanua upatikanaji wa umeme wa kuaminika, nafuu, na endelevu ili kuendeleza uchumi, kuboresha maisha, na kuunda ajira barani Afrika.
“Tamko la Nishati la Dar es Salaam, lililoidhinishwa kwenye Mkutano wa Nishati wa MISSION 300 Africa, ni hatua muhimu katika kushughulikia pengo la nishati barani Afrika, ambapo zaidi ya watu milioni 600 kwa sasa wanaishi bila umeme.
Ahadi zilizomo katika tamko hili ni sehemu muhimu ya mpango wa MISSION 300, ambao unaleta pamoja serikali, benki za maendeleo, wadau wa sekta binafsi, na mashirika ya kifedha ili kuwaunganisha Waafrika milioni 300 na umeme kufikia 2030,”.
Katika mkutano huo, wadau wa Mission 300 waliahidi zaidi ya dola bilioni 50 kusaidia kuongeza upatikanaji wa nishati Afrika.
Taarifa hiyo ilisema kwa kushughulikia changamoto ya msingi ya upatikanaji wa nishati, MISSION 300 inakuwa msingi wa ajira kwa vijana wa Afrika na chachu ya maendeleo ya baadaye.
Katika kuanza utekelezaji wa MISSION 300 nchi 12 zimethibitisha kuanza Mipango Madhubuti ya Kitaifa ambazo ni Chad, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Liberia, Madagascar, Malawi, Mauritania, Niger, Nigeria, Senegal, Tanzania, na Zambia.
Nchi hizo ziliwasilisha Mikataba ya Kitaifa ya Nishati inayoeleza malengo ya kuongeza upatikanaji wa umeme, kuongeza matumizi ya nishati mbadala, na kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi.
Mipango hii ya kitaifa imewekewa muda maalum, inatokana na data sahihi, imeidhinishwa katika ngazi za juu za serikali, na inalenga kizazi cha umeme kwa gharama nafuu, upanuzi wa mtandao wa umeme, ushirikiano wa kikanda, kuboresha utendaji wa kampuni za usambazaji wa umeme na kuimarisha suluhisho la kupikia kwa nishati safi.
Kwa kutumia teknolojia za ramani za satelaiti na kielektroniki, mipango hii inatambua suluhisho za gharama nafuu za kupeleka umeme kwa maeneo ambayo hayajahudumiwa ipasavyo.
Akizungumza kwenye mkutano huo Rais Samia Suluhu Hassan alisema Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa mkutano huu mkubwa ambao umewapa fursa ya kujadili jinsi wanavyoweza kutimiza ahadi zao kwa wananchi kwa kuwapatia umeme na suluhisho za kupikia nishati safi itakayobadilisha maisha na uchumi.
Pia taarifa hiyo ilisema katika kutekeleza Mikataba ya Kitaifa ya Nishati kutahitaji utashi wa kisiasa, maono ya muda mrefu, na usaidizi kamili wa wadau wa MISSION 300.
Serikali zinajitahidi kwa kuanzisha mageuzi makubwa, yakisaidiwa na ufadhili wa masharti nafuu, ushirikiano wa kimkakati na mashirika ya kifedha na maendeleo ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi.
“Upatikanaji wa umeme ni haki ya msingi ya binadamu. Bila umeme, nchi na watu hawawezi kuendelea,” alisema Ajay Banga, Rais wa Benki ya Dunia.
Na kuongeza kiwa “Lazima tukubali ukweli mmoja: hakuna anayeweza kufanya hili peke yake. Serikali, wafanyabiashara, mashirika ya kifedha, na benki za maendeleo zina jukumu—na kwa kushirikiana pekee tunaweza kufanikisha lengo letu.”
Naye Dk Akinwumi Adesina, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), alisisitiza haja ya kuchukua hatua za haraka ili kuharakisha uelektrifikishaji wa bara hili.
“Mageuzi muhimu yanahitajika ili kuongeza sehemu ya nishati mbadala, kuboresha utendaji wa mashirika ya umeme, kuhakikisha uwazi katika utoaji wa leseni na mikataba ya ununuzi wa umeme, na kuanzisha mfumo wa viwango vya bei unaoakisi gharama za uzalishaji.
Kazi yetu ya pamoja ni kusaidia wakuu wa nchi kuandaa na kutekeleza mipango ya kitaifa ya nishati ambayo itawapatia wananchi umeme wa uhakika,” alisema Adesina.
Katika mkutano huo, washirika walitangaza ahadi zifuatazo za ufadhili ambapo AfDB WB wameahidi kutoa Dola za Marekani bilioni 48 kwa Mission 300 kufikia 2030
Agence Française de Développement (AFD): Euro bilioni 1, Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB): Dola bilioni 1 hadi 1.5, Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (IsDB): Dola bilioni 2.65 na Mfuko wa OPEC: Dola bilioni 1 kusaidia MISSION 300.
Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika zilitangaza kuanzishwa kwa Zafiri, kampuni ya uwekezaji inayosaidia suluhisho zinazoongozwa na sekta binafsi, kama vile mini-grids za nishati mbadala na mifumo ya jua ya nyumbani. Wadau wa msingi wa Zafiri watawekeza hadi dola milioni 300 katika awamu ya kwanza na kuchangisha hadi dola za Marekani bilioni 1 ili kushughulikia pengo la mtaji barani Afrika.
Ahadi hizi za dhati kutoka kwa serikali na wadau wa kimataifa zinaonyesha nguvu ya kipekee ya ushirikiano wa Mission 300. Kwa mageuzi ya serikali, ufadhili ulioimarishwa, na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi, nchi za Afrika zina nafasi ya kubadili mipango kuwa hatua halisi, na kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa mamilioni ya watu.
Kuhusu Mkutano wa Mission 300
Mkutano wa Nishati wa Mission 300 Africa uliandaliwa na Tanzania, Umoja wa Afrika, AfDB, WBG, kwa msaada wa Rockefeller Foundation, Energy Sector Management Assistance Program (ESMAP), Global Energy Alliance for People and Planet (GEAPP), Sustainable Energy for All (SEforALL), na Sustainable Energy Fund for Africa.
Mwisho