Na WAF – Dar es Salaam
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2019 zinaonyesha kuwa, takriban watu milioni 17.9 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya moyo ikiwa ni sawa na asilimia 32 ya vifo vyote duniani ikiwemo Tanzania.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Januari 24, 2025 kwenye uzinduzi wa Kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Oyster Bay Jijini Dar es Salaam.
“Kati ya vifo hivi, asilimia 85 husababishwa na mshtuko wa moyo pamoja na kiharusi, takwimu hizi zinaonyesha ukubwa wa tatizo la magonjwa haya Duniani na Tanzania ikiwemo,” amesema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama amesema kutokana na changamoto hiyo kubwa Duniani Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa kwa kiwango cha kimataifa kwenye vifaa tiba pamoja na mitambo mbalimbali ikiwemo mashine za uchunguzi wa magonjwa kama MRI, CT- Scan pamoja na Ultrasound.
“Katika Taasisi hii ya JKCI, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha usimikwaji wa mashine Tatu za Cathlab carto kwa ajili ya upasuaji kwa njia ya tundu dogo ambapo upasuaji huu umepunguza kwa kiwango kikubwa muda wa mgonjwa kukaa hospitali,” amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali imeendelea kuhakikisha Hospitali zinakuwa na uwezo wa kutoa huduma za matibabu kwa wananchi katika namna mbalimbali ikiwemo programu ya tiba mkoba (Outreach Programe) ijulikanayo kwa jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach programe.
“Upanuzi wa huduma za kibingwa za matibabu ya magonjwa ya moyo katika hospitali zetu za kanda Chato, Hospitali ya Benjamini Mkapa, Hospitali ya Kanda Mtwara na nyinginezo umeonyesha dhamira ya dhati na kutafsiri kwa vitendo dhana ya UTALII TIBA – (Medical Tourism) ambapo watu kutoka mataifa mengine kuja kutibiwa nchini,” amesema Waziri Mhagama
Katika hatua nyingine Waziri Mhagama amesema utekelezaji wa mkakati wa bima ya afya kwa wote unaendelea na huu unakwenda kuwa muarobaini wa changamoto nyingi za upatikanaji wa huduma za afya hapa nchini, “na kwa pamoja tuungane katika kuwaelimisha wananchi umuhimu wa Bima ya afya kwa wote kuwa ndio mkombozi wa huduma za matibabu kwa watanzania,” amesema Waziri Mhagama
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Kisenge amesema Taasisi hiyo wanaweza kuwaona wagonjwa hadi 300 wa upasuaji wa tundu na wagonjwa 800 wa upasuaji wa kifua kwa siku, ambapo wamejiwekea malengo ya kuwaona wagonjwa 3500 wa upasuaji wa tundu kwa mwaka na wagonjwa 900 wa upasuaji wa kifua kwa mwaka.