Home BUSINESS ZAIDI YA MABINTI 15 WANUFAIKA NA MAFUNZO YA USHONAJI KUTOKA ECO WEAR

ZAIDI YA MABINTI 15 WANUFAIKA NA MAFUNZO YA USHONAJI KUTOKA ECO WEAR

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

TAASISI inayojihusisha na utunzaji wa Mazingira ‘Environment Conservation Community of Tanzania(ECCT) kupitia Mradi wake wa ‘ECO WEAR’ inatoa mafunzo ya ushonaji wa nguo,mifuko mbadala na urembo unaotokana taka nguo kwa wasichana yenye lengo kubwa la kuwawezesha kuwa na ujuzi wa kushona sambamba na utunzaji wa mazingira.

Kupitia Mradi huo zaidi ya mabinti 15 kutoka Tabata Kimanga Jijini Dar es Salaam watapatiwa mafunzo hayo kwa Kipindi cha miezi sita na pindi ambapo watamaliza mafunzo hayo wataendelea kusaidiwa katika kuendeleza shughuli zao kwani tayari watakuwa na ujuzi unaowezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Akizungumza leo Desemba 11,2024 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Taasisi ya ECCT Lucky Michael amesisitiza kuwa Mradi huo wa ECO WEAR unaohusisha mabinti wa kike ukilenga kuwapa mafunzo ya ushonaji pamoja na kuwafundisha kutunza mazingira kwa kupunguza uchafuzi wa taka nguo.

“Takwimu zinaonesha kwamba taka zinazotokana na nguo ni namba mbili kuchafua mazingira duniani ,ukiachana na viwanda vya plastiki.Kwa kutambua hilo taasisi ya ECCT tumeona ni vema kuwezesha mabinti hawa ambao wanatokea katika mazingira magumu lakini pia wanatoka katika namna mbalimbali katika jamii ili waweze kupata mafunzo haya na hatimaye waweze kujikwamua kiuchumi lakini watunze na mazingira…

“Kwani tunawafundisha pia suala zima la uchambuzi wa taka kwani sio kila nguo ambayo tunaipata ama mabaki ya vitambaa yanayoshonwa tunatumia yote au nguo zote tunarudisha katika urejeshaji bali tunachambua ili kuona nguo au vitambaa gani tunatumia.

“Pia tunatoa elimu kwa jamii kuhusu utunzaji wa mazingira kwani tunaamini suala utunzaji mazingira ni mtambuka lakini Jamii yetu bado inahitaji elimu zaidi ili wawe wakwetu katika kutunza mazingira,”amesema na kutumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa Serikali za Mitaa yote mitano iliyopo katika Kata ya Kimanga, ofisi ya Kata na Ofisa maendeleo kata kwa kufanikisha kuwapata Wanufaika hao.

Vilevile Michael amesema kupitia hao wasichana wanashirikiana na taasisi ya Arizona Vocational Training Center ambayo imesajiliwa chini ya VETA, hivyo wanatoa mafunzo ya ushonaji pamoja na kuangalia namna wanaweza wakawa wanapata nyenzo za ushonaji.

Pia amesema wanashirikiana na taasisi ya Leaders joint forum kuwezesha mabinti hao kufahamu haki zao hasa katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa mtoto wa kike,haki zake lakini wanawafundisha ujasiriamali , biashara na kurasimisha biashara zao na kusisitiza baada ya mafunzo hayo watakwenda kuanzisha biashara zao.

Hata hivyo amesema katika kuhakikisha wanasimamia biashara zao Taasisi hiyo wanatoa mafunzo ya ujasiriamali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na hasa Women Fund Tanzania (WFT- T)ambao kwa sehemu ya wanafanikisha mafunzo hayo.

Ametoa rai kwa wananchi na wadau mbalimbali waweze kutusaidia kuchangia nguo, kuchangia mabaki ya nguo na vitambaa.Pia wanaomba washonaji,wauza mitumba,taasisi na watu mbalimbali kusaidia kuwapatia mabaki ya nguo na nguo ambazo zimeshatumika ili ziwasaidie katika kufanikisha jitihada zao.

“Kwahiyo tumekuwa sehemu ya kutunza mazingira lakini kama wanawake tunakwenda kutengeneza nguo kwa kuziongezea thamani lakini sio nguo tu tunatengeneza urembo unaovaliwa kwa mfano hereni ,kibanio cha Nywele, tunatengeneza mifuko mifuko ya kubebea laptop.

“Kwahiyo sisi kama wadau wa mazingira tunasaidia hawa mabinti waweze kupata ujuzi wa kuzalisha mifuko ambayo inatumika katika mikutano yetu mbalimbali na unaponunua bidhaa zetu tayari unakuwa umemkomboa kiuchumi lakini umeyatunza mazingira

“ECCT huwa tunakauli mbiu yetu inasema Pamoja tuyatunze mazingira tukimaanisha kila mmoja wetu anayo nafasi na anapaswa kuyatunza mazingira,sio Serikali,sio taasisi au Kampuni fulani bali ni jukumu letu wote.”

Kwa upande wake Nyanzobe Makwaiya ambaye ni Mratibu wa Mradi wa ECO WEAR amesema kuwa mabinti walioko katika Mradi huo ni wenye umri kuanzia miaka 18 mpaka miaka 35 na wote wametoka Kata ya Kimanga kwasababu ndio Kata ambayo wameichagua kufanya mradi huo.

Ameongeza kuwa kupitia Mradi huo walilenga mabinti ambao wanapitia ukatili au wako nyumbani na hawajishughulishi na shughuli yoyote kwa kipindi hiki ,hivyo wameamua ujuzi huo ambao utawawezesha kujikwamua kiuchumi .

Amefafanua wameamua kujikita katika taka Nguo kwasababu ni taka ambazo hazijapewa kipaumbele na Taasisi nyingine lakini takwimu zinaonesha asilimia 0.8 ya nguo ambazo zinapelekwa dampo la Pugu ni taka nguo na mwisho wa siku zinaishia kuchomwa ambapo hiyo inakuja kuleta madhara katika mazingira.

Kwa upande wa wanufaika wa Mradi huo Hamisa Hussein , Aneth Benezeth na Salma Mwishehe wamesema wanaaamini baada ya mafunzo hayo watakuwa na ujuzi wa kushona na hivyo kuwa na fursa ya kujiendeleza kiuchumi sambamba na kutunza Mazingira.

Wamesema tayari wameshaanza kufahamu kushona na wanaamini baada ya miezi sita watakuwa na uwezo mkubwa katika ushonaji wa nguo na mifuko mbadala huku wakiishukuru Taasisi hiyo kwa kuwapa nafasi hiyo kwani walikuwa mtaani na hawakuwa na shughuli yoyote ya kuwaingizia kipato.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here