Wizara ya Afya kuendelea ushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwezesha maendeleo katika sekta ya Afya.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Ntuli Kapologwe wakati Kikao kazi cha kuandaa Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa miaka mitano wa kituo cha Afya Call Center 199 kinachofanyika Jijini Dar es Salaam.
Dkt.Kapologwe amesema kuwa Mpango mkakati huo ni muhimu kuendana na malengo ya Serikali ikiwemo Dira ya Taifa ya maendeleo 2050 ambayo rasimu yake ilizinduliwa Desemba 10 na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Tumezindua rasimu yasa Dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2050 lakini pia hivi sasa tupo katika mchakato wa kupitia Mpango mkakati wa miaka mitano wa sekta ya Afya hivyo niwaombe wajumbe muweze kupitia nyaraka hizo ili kuhakikisha mpango huu wa utekelezaji unaenda sambamba na mipango mingine ya nchi” amesema.
Pia Dkt .Kapologwe amesisitiza kuwa Mpango huu wa utekelezaji qwa miaka mitano wa Afya Call Center utasaidia kuboresha ufanisi wa kituo.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ona Machangu amesema Kituo cha Call Center kilianzishwa kutokana mahitaji ya kujibu hoja mbalimbali za wananchi wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 Lakini sasa ni wakati wa kuona ni kwa namna gani kituo kinachangia katika utoaji wa huduma za afya hususani eneo la Elimu ya Afya kwa umma
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Village Reach Bi Jessica Mayenda amesema kuwa kituo cha Afya Call Center ni mfano wa kuigwa barani Afrika kulingana na uwekezaji mkubwa uliofanyika hivyo mpango mkakati utasaidia kukifanya kituo cha Afya Call Center kuwa kituo cha umahiri barani Afrika.
Kituo cha Afya Call Center ni kituo cha simu kilicho chini ya wizara ya Afya kinachosimamiwa na Idara ya huduma za kinga, katika sehemu ya Elimu ya Afya kwa umma.