Dkt. Nchemba alitoa wito huo leo, Desemba 10, 2024, wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024, lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, Dar es Salaam. Jukwaa hilo linalenga kujadili fursa na hatua za kuboresha sekta ya fedha, huku likiwakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi.
KUKEMEA RIBA KUBWA KWENYE MIKOPO
Waziri Nchemba alisisitiza kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na taasisi zake, itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya taasisi zinazotoa mikopo yenye riba kubwa, maarufu kama “mikopo kausha damu.” Alieleza kuwa riba hizo zinadhalilisha wakopaji na kuwaweka katika hatari ya kupoteza mali zao.
“Hatutaacha kuchukua hatua kwa taasisi zinazotoa mikopo kwa riba za kupandisha shinikizo la damu. Tunataka sekta ya fedha iwe ya utu na inayochangia ustawi wa wananchi,” alisema Dkt. Nchemba.
WADAU WA SEKTA YA FEDHA WASHIRIKI JUKWAA HILO
Jukwaa hilo limewaleta pamoja wadau kutoka sekta za benki, taasisi za fedha, kampuni za bima, vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS), vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha, na vyama mwavuli vya sekta ya fedha.
Viongozi mbalimbali walihudhuria, akiwemo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Sauda Msemo, na Mkurugenzi wa Hifadhi ya Jamii, Bw. Festo Fute.
UMUHIMU WA ELIMU YA UJASIRIAMALI
Prof. Adolf Mkenda alipongeza Wizara ya Fedha kwa kuandaa jukwaa hilo na kuonesha mshikamano wa sekta za elimu na fedha katika maendeleo ya kiuchumi. Alifichua kuwa Wizara yake imeandaa mtaala mpya wa elimu unaojumuisha masuala ya ujasiriamali na biashara kwa wanafunzi.
“Mtaala huu mpya unalenga kuwajengea wanafunzi maarifa ya kujikwamua kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika sekta ya fedha. Tunahitaji kizazi kinachoelewa uchumi wa kisasa,” alisema Prof. Mkenda.
Kwa ujumla, Jukwaa hili limeonyesha dhamira ya dhati ya serikali na wadau wa sekta ya fedha kushirikiana katika kuboresha huduma na kufanikisha maendeleo endelevu ya kiuchumi nchini.
.