Baadhi ya watia nia nafasi ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika Kijiji cha Litapwasi wakiwa katika zoezi la kuchaguliwa kwenye mkutano wa hadhara.
Katika Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, Mikutano ya hadhara imeanza katika maeneo mbalimbali Mkoani Ruvuma kwa lengo la kufanya uchaguzi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.
Wakizungumza katika mikutano hiyo, baadhi ya watia nia ya kugombea nafasi hizo wamesema wameamua kuwania nafasi za Huduma za Afya Ngazi ya Jamii kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya katika Huduma Afya ya Msingi.
“Kuanzisha Mpango Jumuishi utaleta chachu katika eneo la lishe na nimeamua kuwania kwa sababu kazi ambayo naipenda na ipo moyoni nitajitahidi kutoa elimu ya Afya kuhusu lishe katika kupambana na udumavu” amesema Magreth Mapunda kutoka Kijiji cha Liganga .
“Nilikuwa kwenye Kamati ya Huduma za Afya ya Kijiji hapo nyuma nikagundua changamoto zilizopo nikaamua kuwania nafasi hii nashukuru Serikali kwa kuleta Mpango huu nitahakikisha natoa elimu ya Afya kuhusu usafi wa Mazingira katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko” amesema Viana Severine .
“Ninawania nafasi hii kwa Sababu ninajiamini pia matarajio yangu ni kuhudumia wanajamii na kutunza siri zao” amesema Regina Komba.
Bushiri Tindwa ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Litapwasi Wilaya ya Songea ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuleta Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii .
“Kupitia Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wananchi watapata huduma za Afya katika maeneo wanayoishi iwe majumbani wanapata elimu ya Afya namna ya kujikinga na magonjwa hivyo naishukuru sana Serikali “amesema.