Na Mwandishi wetu
Serikali imekusanya jumla ya shilingi bilioni 325.3 ikiwa ni mapato yanayotokana na shughuli za mikataba iliyoingiwa kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na DP World, ikijumuisha tozo ya pango (land rent), tozo ya mrabaha (royalty), na Ardhi.
Hayo yameelezwa leo Desemba 19, 2024, jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali yaliyoyekelezwa na serikali.
“Katika kipindi cha miezi mitano (Aprili hadi Septemba 2024) tangu DPW Dar es Salaam waanze kuendesha Gati 0-7 katika Bandari ya Dar es Salaam, Serikali imeshakusanya jumla ya shilingi bilioni 325.3 ikiwa ni mapato yanayotokana na shughuli za mikataba iliyoingiwa kati ya TPA na DP World, ikijumuisha tozo ya pango (land rent), tozo ya mrabaha (royalty), na Ardhi,” amesema Msigwa.
Ameendelea kusema kuwa, kutokana na kuongezeka kwa mapato na kupungua kwa gharama za uendeshaji kufuatia maboresho yaliyofanyika, serikali, kupitia TPA, imeanza uwekezaji katika miradi yenye thamani ya TZS 1.922 trilioni (USD 686.628 milioni) kwa kutumia makusanyanyo yanayopatikana.
“Miradi hii ni Ujenzi wa Kituo cha Kupakulia Mafuta (SRT), Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao (Mtwara) pamoja na Ujenzi wa Gati za Majahazi (Dhow Wharf) Dar es Salaam. Kuunganishwa kwa mifumo ya forodha (Tanzania Customs Integrated System – TANCIS) na ile ya bandari (Tanzania Electronic Single Window System-TeSWS),” amesema Msigwa.
Aidha, maboresho hayo yamewezesha kupunguzwa na kuondolewa kwa mifumo iliyokuwa inafanana na hivyo kupunguza muda wa kuondoa mizigo bandarini, kuongeza uwazi na kurahisisha mawasiliano.