Na Mwandishi Wetu.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema timu ya maandalizi ya hatua za mchakato ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, imekamilisha rasimu ya kwanza ya dira hiyo ambayo imejumuisha hatua mbalimbali na maoni ya wananchi nchi nzima.
Amesema kwasasa ipo rasimu ya kwanza, lakini hatua inayofuata ni kuzinduliwa kwa rasimu mpya na baada ya kuzinduliwa, mchakato utaingia awamu ya pili ya ukusanyaji wa maoni ya ziada kutoka kwa wadau, na kuipeleka kwa wananchi kupitia mitandao na vyanzo vingine ili waweze kusoma na kutoa maoni yao.
Waziri huyo amesema wananchi watakabidhiwa rasimu na maudhui yaliyojitokeza, kisha wataulizwa kama wana maoni na sehemu geni ya kuboresha.
Profesa Mkumbo amesema hatua itakayofuata ni uzinduzi wa Rasimu ya Pili ya Dira utakaofanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Januari 18,2025, na kuhitimisha mchakato wa wananchi kabla ya kuendelea na hatua nyingine ili kukamilishwa kuandikwa kwa dira yenyewe.
“Rasimu ya Pili itajumuisha maoni yote ya wadau yaliyokusanywa katika hatua ya uhakiki. Hii ni hatua muhimu ya kuhakikisha kwamba Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inakuwa mchakato wa wananchi.”
Tathmini hiyo iliyozinduliwa rasmi Desemba 9,2023 na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua rasmi nyenzo za kukusanya maoni ya wadau, ambayo ni kukusanya maoni ya wananchi na wadau wa maendeleo.
Amesema hadi kufikia Oktoba 2024, jumla ya wananchi na wadau 1,170,970 walitoa maoni yao kwa njia za tafiti katika ngazi ya kaya 15,483, ujumbe kwa njia ya simu (USSD) 1,118,978, tovuti 13,459, akongamano 12 yaliyohudhuriwa na watu 22,779, mahojiano maalum na viongozi mbalimbali waliopo madarakani na waliostaafu 44, mikutano na semina 220 na nyaraka zilizokusanywa 33.
Pamoja na hayo walipata nafasi ya kujifunza kutoka nchi mbalimbali zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo kutoka mabara ya Afrika, Asia, Ulaya na Amerika.
Amesema kuwa, matamanio na matarajio ya wananchi na wadau ni katika maeneo makubwa matano ni uchumi imara, unaostawi na unaoboresha maisha yao, huduma bora za jamii (elimu na afya), utawala bora, utoaji haki, ulinzi na usalama, maendeleo ya teknolojia na ubunifu na ulinzi na matumizi endelevu ya raslimali za taifa.
Waziri Mkumbo amesema wananchi na wadau walitaja sekta tano za kuzingatiwa kama vipaumbele vya kitaifa kuelekea mwaka 2050 ambazo ni kilimo, uzalishaji viwandani (kuongeza thamani, iundombinu, huduma bora za jamii, madini, mafuta na gesi.
Amesema kwa kuzingatia maoni ya wananchi na wadau mbalimbali, taarifa za kitafiti na uzoefu kutoka nchi mbalimbali zilizopiga hatua kubwa za kimaendeleo, Kamati Kuu ya Kitaalam imeandaa Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050) itazinduliwa rasmi Desemba 11,2024 katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar na mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi”
Amesema uzinduzi wa Rasimu ya Dira 2050 utakwenda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya kukusanya maoni ya wadau itakayohusu maoni ya uhakiki wa Rasimu ya Dira 2050 (validation).
Waziri Profesa Mkumbo amesema Januari – Machi 2025 Rasimu ya Dira 2050 itajadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika vyombo vya serikali (Makatibu Wakuu, Tume ya Taifa ya Mipango na Baraza la Mawaziri), wakati Aprili-Mei 2025 itapokelewa, kujadiliwa na kuidhinishiwa rasmi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzinduwa rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Mei/Juni 2025.