Home LOCAL MHANDISI SEFF AWASHUKURU WOTE WALIOMPIGIA KURA TUZO ZA ‘CEO’ BORA 2024

MHANDISI SEFF AWASHUKURU WOTE WALIOMPIGIA KURA TUZO ZA ‘CEO’ BORA 2024

#Awataka watumishi kuchapa kazi kutimiza lengo la Serikali

Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za VIjijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amewashukuru Watanzania wote waliojitokeza na kumpigia kura wakati akiwania tuzo za Mtendaji/Mkurugenzi Mkuu Bora wa mwaka 2024 kati ya Wakurugenzi 100 walioteuliwa kuwania tuzo hizo (Top 100 Executive List Awards) na yeye kuibuka kinara.

Mhandisi Seff ameyasema hayo leo tarehe 3/12/2024 jijini Dodoma wakati akiongea na watumishi waTARURA Makuu mara baada ya kuwasili ofisi za Taasisi hiyo zilizopo Mji wa Serikali Mtumba.

Mhandisi Seff amewashukuru watumishi wote kwa ushirikiano wao katika utendaji kazi wa Taasisi hiyo na hivyo kumfikisha hapo alipo “Hili sio jambo dogo, ni jambo la kumshukuru Mungu sana. Naomba tuendelee kumshukuru Mungu ili Taasisi yetu iendelee kufanya vizuri”.

Aidha, amewataka watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kutimiza malengo ya Serikali pamoja na kuendeleza yale ambayo yeye ameyafikia “Sasa hivi tumepata sifa hii kubwa ila kazi kubwa tuliyonayo ni kuilinda sifa hii. Na mimi naona timu iliyopo hapa inaweza kuilinda sifa hii iwe nipo au hata nisipokuwepo”, amesema.

Hata hivyo, amesema kwamba Serikali inaendelea kuthamini kazi kubwa inayofanywa na TARURA hivyo amewasihi watumishi wote kuendelea kuchapa kazi ili kuhakikisha Taasisi inabaki na sifa iliyopo.

Naye, Mkurugenzi wa Barabara, Mhandisi Venant Komba amempongeza Mtendaji Mkuu huyo na kusema kuwa Uongozi wake umekuwa ni msaada mkubwa kwa viongozi wengine wa chini yake ambapo ameacha milango wazi wa kila mtumishi kumsikiliza muda wote na kuahidi wataendelea kumpa ushirikiano katika majukumu yake.

Pia, Mhasibu Mkuu, CPA. Jacob Nyaulingo amempongeza Mtendaji Mkuu kwa kuitwaa tuzo hiyo na kumuelezea Mtendaji Mkuu kama mtu anayependa mabadiliko ambayo yamepelekea kutengeneza mfumo wa malipo, mapato pamoja na uanzishaji wa hatifungani ya miundombinu ya barabara (Samia Infrastructure Bond) ambayo inaenda kuwasaidia wakandarasi wanaofanya kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara za Wilaya zilizo chini ya TARURA.

Akitoa salamu kwa niaba ya Watumishi wa TARURA Mtunza Kumbukumbu Msaidizi, Bi. Sekela Fumbo amempongeza Mtendaji Mkuu kwa kuchaguliwa kuwa ‘CEO’ Bora wa Mwaka 2024 na kuahidi kwamba watumishi wataendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uaminifu ili Taasisi izidi kufanya kazi vizuri zaidi ya hapo ilipo.

Wakati huo huo, Dereva Mkuu, Bw. Assery Masawe amesema kwamba wanajivunia kumpata Kiongozi ambaye anafanya kazi kwa kiwango kikubwa licha ya TARURA kuwa na muda mfupi tangu kuanzishwa kwake, hivyo wanampongeza na kumtia moyo aendelee kuwaongoza katika kuiendeza Taasisi yao vyema.

http://MHANDISI SEFF AWASHUKURU WALE WOTE WALIOMPIGIA KURA TUZO ZA ‘CEO’ BORA WA MWAKA 2024

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here