Home LOCAL M/KITI WA KAMATI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU (SMZ) APONGEZA SERIKALI

M/KITI WA KAMATI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU (SMZ) APONGEZA SERIKALI

DAR ES SALAAM

Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Machano Ali Machano, amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi zao za kutafuta fedha zinazowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Machano alitoa pongezi hizo leo wakati wa ziara ya Kamati hiyo kutembelea miradi ya TASAF katika eneo la Mabwepande, jijini Dar es Salaam. Alieleza kuwa zaidi ya kaya milioni moja zimenufaika na huduma za TASAF, hatua ambayo imepunguza mzigo kwa serikali katika kupambana na umasikini na kuchochea maendeleo ya wananchi.

“Kitendo cha kuwatumikia wananchi kwa kiwango hiki kinadhihirisha kuwa tuna viongozi waadilifu na wenye mapenzi ya dhati kwa watu wao. Hili ni jambo la kujivunia, na tunapaswa kumwombea dua Mheshimiwa Rais wetu,” alisema Machano.

Machano aliongeza kuwa mafanikio yaliyopatikana kupitia TASAF ni fahari kwa nchi, akitaja kwamba miradi mingi imetekelezwa Zanzibar, ambapo mabilioni ya shilingi yametumika katika awamu tatu za mpango huo. Alihimiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano mzuri ili kuhakikisha wafadhili wanaridhika na kukubali kuingia katika Awamu ya Nne ya mpango huo.

“Kwa miezi michache iliyobakia, tunahitaji utulivu na umakini mkubwa ili kuhakikisha kazi za TASAF zinasonga mbele. Tunapaswa pia kuwaombea viongozi wetu afya njema na maisha marefu, ili waendelee kusimamia maendeleo haya,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Islam Seif Salum, alisema mpango wa sasa wa TASAF unatarajiwa kukamilika Septemba 2025.

“Mradi huu unawagusa moja kwa moja wananchi wa hali ya chini, na kutekelezwa kwake kunachangia kujenga siasa nzuri nchini. Tunapaswa kuhakikisha huduma za TASAF zinaendelea bila kusita, hasa tunapokaribia kuingia katika awamu mpya,” alisema Salum.

Katibu Mkuu alisisitiza umuhimu wa mipango thabiti katika kipindi hiki cha mpito ili kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanadumishwa na kuimarishwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here