Home LOCAL KUWENI BARAKA, SIO KITUNGUU KUWATOA MACHOZI WENGINE – DKT. BITEKO

KUWENI BARAKA, SIO KITUNGUU KUWATOA MACHOZI WENGINE – DKT. BITEKO

* Amwakilisha Rais Samia hafla ya kutabaruku kanisa SDA- Magomeni*

*Ataka watu kutengenezeana furaha badala ya kuumizana

* Ahimiza Mshikamano wa Taifa ili kuleta maendeleo

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kujenga misingi ya kusaidiana kuheshimiana na kuvumiliana ili kufanikisha malengo wanayojiwekea kimaendeleo.

Dkt. Biteko ametoa rai hiyo leo Desemba 15, 2024 Jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni maalum katika Hafla ya Kutabaruku Jengo la Kanisa la Waasventista Wasabato, Magomeni.

Amewahimiza waumini na Watanzania kwa ujumla kuboresha huduma za jamii na kuwekeza katika mipango itakayowezesha kukidhi mahitaji na kupata Taifa endelevu.

“ Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan siku zote amekuwa akisisitiza maridhiano, uhimilivu, mabadiliko na kuimarisha amani yetu ili jamii iweze kupata maendeleo na kustawi” amesema Dkt. Biteko

Aidha, amewataka waumini kuendeleza moyo wa kujitolea kwa ajili ya uwekezaji na ujenzi wa miundombinu ya maendeleo kama vile kanisa na miradi mingine ya kijamii.

Amesema, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wake kuhakikisha kwamba misingi ya malezi na ushirikiano inayowekwa inafanikiwa.

“ Wametajwa baadhi ya watu waliofanikisha ujenzi wa kanisa hili la Magomeni, lakini pia wapo ambao hawakutajwa kwa kuwa hawakuwa tayari kutajwa na hii ndiyo sababu kwao kutotajwa, sasa tuanze upya kila mmoja ajitahidi kufanya jambo la kheri kwa mwenzie badala ya kumuumiza,” ameongeza kuwa tuwe baraka kwa watu wengine na sio Kitunguu cha kuwatoa watu machozi machoni” amesisitiza Dkt. Biteko

Kwa upande wake, Mch. Dkt. Joel Okindo, Msaidizi wa Mwenyekiti wa Divesheni ya Mashariki na Kati amewaka waumini kujenga moyo wa kujitolea katika masuala ya maendeleo ili kutimiza azima ya uumbaji.

Amesema ujenzi wa Kanisa la SDA – Magomeni ulianza takribani miaka 12 iliyopita na ujenzi huo umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 kutokana na michango ya waumini, wafadhili na viongozi mbalimbali.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila ametumia jukwaa hilo kutoa ufafanuzi kuhusu madai ya mtu mmoja anayedaiwa kutekwa ambapo amesema mtu huyo alitumia mbinu hizo baada ya kuuza gari alilokuwa ameazima.

“ Mhe. Naibu Waziri Mkuu, Dar es Salaam ni salama na huyu mtu anayedaiwa kutekwa ni kwamba “amejiteka” baada ya kuazima gari na kuliuza, Gari tayari tunalo na huyo mtuhumiwa atatokea hadharani hivi karibuni kuelezea kilichotokea.” amesema Chalamila.

      

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here