Home LOCAL KUKUA KWA SEKTA YA UTALII NCHINI NI MATUNDA YA RAIS DKT. SAMIA

KUKUA KWA SEKTA YA UTALII NCHINI NI MATUNDA YA RAIS DKT. SAMIA

Na Emmanuel Buhohela

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewaongoza Viongozi Wakuu wa Wizara akiwemo Naibu Waziri Mhe. Dastan Kitandula kupokea rasmi Tuzo ya Kivutio Bora cha Utalii wa Safari Duniani 2024.

Akizungumza wakati wa kupokea tuzo hiyo leo Disemba 03, 2024 jijini Dodoma katika semina ya siku mbili inayoshirikisha Maafisa Wanyamapori wa Wilaya nchini, Waziri Chana amesema Rais Dkt. Samia amekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwemo Sekta ya Utalii.

Mhe. Chana ameongeza kuwa kwa Tanzania kuendelea kutwaa tuzo nyingi ulimwenguni ni kutokana na jitihada, maono na matunda ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza vivutio vya utalii kwa vitendo ndani na nje ya Tanzania.

“Tanzania kutwaa tuzo ya Kivutio bora cha Utalii ni kutokana na Juhudi na Maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuthamini na kutangaza sekta ya utalii kupitia filamu za “Tanzania The Royal Tour” na “Amazing Tanzania”.

Akizungumza wakati wa Kumkaribisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) amesema tangu kuingia kwa Rais Samia madarakani amekua mstari wa mbele katika kukuza Sekta hiyo kwa kushiriki Filamu ya “Tanzania The Royal Tour” na “Amazing Tanzania” ambazo zimechangia ongezeko la watalii kufikia asilimia 96 kwa takwimu za mwezi Mei 2024.

“Mhe. Rais Dkt. Samia ameimarisha bajeti ya uendeshaji wa shughuli za uhifadhi na utangazaji utalii kwa kurejesha Fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Utalii” amesema Mhe. Kitandula.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema tuzo hiyo imekua ni heshima kubwa kwa Tanzania kwa kuwa inakwenda kuwa chachu ya ongezeko la utalii nchini na kuahidi kuendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa watalii kwa kuongeza vivutio vipya.

Hafla hiyo ya kupokea tuzo imehudhuriwa na Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakurugenzi/ Wakuu wa Vitengo na baadhi ya watumishi.

http://KUKUA KWA SEKTA YA UTALII NCHINI NI MATUNDA YA RAIS DKT. SAMIA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here