Home LOCAL WAZIRI CHANA AZINDUA MIRADI YA UTALII YA MILIONI 904 SERENGETI

WAZIRI CHANA AZINDUA MIRADI YA UTALII YA MILIONI 904 SERENGETI

Na Happiness Shayo – Serengeti

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amezindua miradi ya kuendeleza utalii ikiwemo Mradi ya Barabara ya Utalii km22 uliogharimu takribani 761.3 na Mradi wa ujenzi wa Vituo Viwili vya kupokea na kukagua wageni(Ikona Gate na Visitors Gate) uliogharimu takribani shilingi milioni 143.5 katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Ikona iliyopo Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara.

Uzinduzi huo umefanyika leo Novemba 15,2024 katika Jumuiya ya Hifadhi ya Ikona Serengeti Mkoani Mara.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mhe. Chana ameitaka jumuiya hiyo kuisimamia na kuitumia vyema miradi hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ya kukuza utalii huku akisisitiza maadili katika utendaji kazi.

Natoa rai kwa Wafanyakazi kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu ya ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za Taifa” amesisitiza Mhe. Chana.

Aidha, ameipongeza Menejimenti na Jumuiya ya Ikona huku akitoa rai kuendelea kushirikiana kwa karibu na Halmashauri za Wilaya, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kutekeleza majukumu yao.

Naye, Mhasibu wa Jumuiya ya Ikona, Mariam Magessa amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo, imefanikiwa kupunguza matukio ya ujangili hivyo kupelekea ongezeko la wanyamapori huku ikivutia shughuli za utalii na wawekezaji.

Matokeo chanya ya uhifadhi yamepelekea kupata jumla ya wawekezaji 9 ambapo 8 wamewekeza kwenye utalii wa picha na mmoja kwenye utalii wa uwindaji” amesisitiza Mariam na kusema kuwa hiyo imekuwa ni sehemu ya mapato ya Jumuiya hiyo.

Jumuiya ya Ikona ilianzishwa mwaka 2005 kwa dhumuni la kuendeleza uhifadhi na Usimamizi endelevu wa Maliasili na vivutio vya utalii kama njia ya kukuza uchumi na hivyo kupunguza kiwango cha umaskini kwa wananchi wanaoishi katika vijiji wanachama.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here