Home LOCAL WAZIRI CHANA AKUTANA NA BALOZI WA URUSI NCHINI TANZANIA

WAZIRI CHANA AKUTANA NA BALOZI WA URUSI NCHINI TANZANIA

Na Happiness Shayo- Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Mhe. Andrey Avetisyan,kuhusu kushirikiana katika Sekta ya Maliasili na Utalii.

Kikao hicho kimefanyika leo Novemba 18,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na umuhimu wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Urusi na Tanzania na kutangaza Tanzania kupitia mawakala wa utalii wa Urusi kwa kuratibu ziara za mafunzo ya utalii (Familiarization Trips).

Pia, kikao kilijadili suala la kushirikiana na kubadilishana ujuzi katika uandaaji wa Maonesho ya kimakumbusho baina Makumbusho ya Taifa la Tanzania na Makumbusho ya Urusi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Chana ameweka bayana kuwa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii iko tayari kushirikiana na Urusi katika Taasisi zake zinazohusiana na masuala ya maliasili na utalii huku akisisitiza “Tunataka kutangaza Utalii wa Tanzania duniani kote na Urusi ni mojawapo ya Soko la Watalii”.

Naye, Mhe. Avetisyan alipendekeza kuwa Tanzania itangaze vivutio vya Tanzania kwa soko la Urusi, hasa utalii wa wanyamapori sababu watalii wengi kutoka Urusi wamekuwa wakipendelea zaidi utalii wa fukwe na kwamba nchi zote mbili ziweke mikakati ya pamoja ya masoko ili kuvutia watalii wa Kirusi kuja Tanzania ikiwema kutafsiri filamu ya Royal Tour kwa Kirusi.

Aliongeza kuwa Urusi kwa sasa wako katika mchakato wa kuanzisha mafunzo ya lugha na tamaduni za Kirusi kwa wataalamu wa utalii wa Tanzania ambapo kwa kuanzia wataanza na Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika MWEKA na Chuo cha Taifa cha Utalii Tawi la Arusha.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkuu wa chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt Florian Mtei, Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Gwakisa Kamatula, Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania ,Vivian Temi na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi Bodi ya Utalii Tanzania, Violeth Limbu

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here