Home INTERNATIONAL TANZANIA NA UTURUKI KUSHIRIKIANA SEKTA YA MALIASILI NA UTALII

TANZANIA NA UTURUKI KUSHIRIKIANA SEKTA YA MALIASILI NA UTALII

Na Happiness Shayo- Dar es Salaam

Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Uturuki zimekubaliana kushirikiana kukuza Sekta ya Maliasili na Utalii lengo ikiwa ni kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchi hizo mbili.

Hayo yamebainika leo Novemba 19,2024 wakati wa kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dkt. Mehmet Gulluoglu kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni ushirikiano kati ya bodi za utalii za Tanzania na Uturuki katika utangazaji wa maeneo ili kuongeza watalii, kushirikiana na Shirika la Ndege la Uturuki kwa ajili ya kukuza na kuhamasisha watalii kuelekea Tanzania na kuanzisha ubia kwa matukio ya Kimataifa ya Utalii ambayo Bodi ya Utalii Tanzania inaandaa au kushiriki ikiwa ni pamoja na maonyesho ya Swahili International Tourism Expo (S!TE).

Waziri Chana alitumia fursa hiyo kunadi maeneo ya uwekezaji ya Tanzania na kukaribisha wawekezaji kutoka Uturuki kuwekeza katika huduma za malazi, usafiri na utalii, mashirika ya ndege, biashara ya uendeshaji wa utalii, vituo vya mikutano na uwindaji wa kitalii.

Napendekeza Tanzania na Uturuki kukuza ushirikiano kati ya sekta binafsi ya nchi hizo mbili ili kuweza kufanya kazi kwa pamoja katika masuala ya biashara ya utalii na uwekezaji” Mhe. Chana amesisitiza.

Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dkt. Mehmet Gulluoglu amesema Uturuki iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kukuza Sekta ya Maliasili na Utalii huku akisisitiza kuwa Tanzania inavutia na imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Florian Mtey, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Eliud Mtailuka, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Glory Mndolwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Gwakisa Kamatula.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here