Home INTERNATIONAL TANZANIA NA AFRIKA KUSINI KUFANYA TAFITI ZA PAMOJA

TANZANIA NA AFRIKA KUSINI KUFANYA TAFITI ZA PAMOJA

NA FARIDA MOROGORO

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia inaandaa mpango wa pamoja wa mashirikiano baina ya Tanzania na Afrika Kusini wa kubadilishana wataalamu na kufanya tafiti za pamoja hali itakayosaidia kuongeza wigo wa ajira kwa Watanzania na maendeleo kati ya nchi hizi mbili.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Ladislaus Mnyone akiwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwenye ziara ya siku moja na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Afrika ya Kusini Mhe. Dkt. Bonginkosi “Blade” Nzimande aliyeambatana na ujumbe wake.

Amesema endapo ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Afrika ya Kusini katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu utaboreshwa basi utaleta maendeleo kwa pande zote mbili “ kupitia mpango huu tunaouandaa wa pamoja tunatamani tupate wanafunzi wanaotoka Afrika ya Kusini kuja Tanzania”. Amesema Prof. Mnyone.

Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Afrika ya Kusini Mhe. Dkt. Bonginkosi “Blade” Nzimande amesema ni muhimu kuwepo kwa ushirikiano kati ya nchi yake na SUA katika maeneo mbalimbali kama Utafiti, Teknolojia na Programu za kubadilishana uzoefu kwa wanafunzi na wataalamu ili kuhakikisha kunakuwa na maendeleo katika sekta ya kilimo na kuleta maendeleo kwa watu wake.

Waziri huyo wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu amesema endapo nchi hizi mbili zitafanya tafiti mbalimbali kwa pamoja zinaweza kuja na matokeo ambayo si tu yatazisadia nchi hizo mbili bali Afrika kwa ujumla.

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kusini itaangalia uwezekano wa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Afrika ya Kusini kuja kusoma katika vyuo vilivyopo Tanzania ikiwa ni pamoja na SUA

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema ni matumaini yao kuwa katika siku za usoni watapata wanafunzi kutoka Afrika ya Kusini na hasa kama wataondoa mtazamo hasi wa elimu inayotolewa katika vyuo vya Tanzania ikiwa ni pamoja na SUA kwani chuo hicho kinafanya vizuri kwa kufundisha na kutoa wataalamu mbalimbali katika maeneo mengine ya Afrika.

Amesema endapo kutakuwa na ufadhili unaotolewa kwa wanafunzi kutoka Afrika ya Kusini watakuja na kupata elimu na ujuzi bora na huenda hata wakatamani kubaki nchini kutokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na amani na utulivu uliopo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here