Tanzania inatarajia kuungana na nchi zaidi ya 50 duniani katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, yanayochangia uharibifu wa mazingira kwa ujumla na wakati huo ikiendelea kukuza utalii.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania Bw. Ernest Mwamaja kwenye Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) Baku, Azerbaijan,
Amesema takriban asilimia 8.8 ya uharibifu wa mazingira unachangiwa na usafiiri wa anga ambao unatumiwa zaidi katika shughuli za utalii hivyo hatua hiyo itasaidia katika kupunguza changamoto hizo.
Bw. Mwamaja amefafanua kuwa Mkutano wa COP29 umejumuisha sekta ya utalii tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma jambo ambalo litaleta faida kwa Tanzania kwani wajumbe watakuwa wanapata wasaa wa kujadili na kupata majawabu ya athari za mazingira.
Aidha, mkurugenzi huyo amnepongeza Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ni imeratibu ushiriki wa mkutano huo mkubwa duniani na kuwezesha wizara, taasisi na wadau mbalimbali kushiriki.
Katika hatua nyingine, Tanzania imeshiriki mkutano wa pembezeno ili kujadili umuhimu wa ajenda ya milima kuendelea kujadiliwa na kuingizwa rasmi kama ajenda ya COP29.
Mkutano huu wa pembezeni umeandaliwa na Serikali ya Krygyzstan, Andorra na Bhutan pamoja na Umoja wa KIRDARC.
Nchi zote katika kutoa michango zimeonyesha umuhimu wa mifumo ikolojia ya milima na namna inavyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. Athari hizo ni kama vile kupotea kwa theluji, bioanuwai, kutokea kwa maporomoko ya ardhi na kukauka kwa vyanzo vya maji.
Mada zilizozojadiliwa ni pamoja na namna Tanzania inachukua hatua kuhakikisha ekolojia na mazingira ya milima nchini inasimamiwa na mazingira yake kutunzwa.
Hii ikiwemo na kuwa na sera, sheria na mifumo ya kitaasisi inayosimamia madhubuti utunzaji huo wa ikolojia na mazingira ya milima nchini.