Home LOCAL SERIKALI YATENGA BILIONI 2.9 UKARABATI WA CHUO CHA MAAFISA TABIBU MASWA

SERIKALI YATENGA BILIONI 2.9 UKARABATI WA CHUO CHA MAAFISA TABIBU MASWA

Na WAF – Simiyu

Serikali kupitia Wizara ya Afya, imetenga Shilingi Bilioni 2.9 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya Chuo cha Maafisa Tabibu kilichopo wilayani Maswa, mkoani Simiyu.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Novemba 29, 2024 katika Mahafali ya 48 ya chuo hicho, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa chuoni hapo, ambapo ujenzi unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba mwaka wa fedha 2024/25.

Tayari Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 2.9 kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya chuo hiki. Hadi kufikia mwezi wa tisa mwakani, tunatarajia ujenzi utakuwa umekamilika, hali ambayo itasaidia kubadilisha mandhari na mwonekano wa chuo hiki,” amesema Dkt. Mollel.

Kauli hiyo ya Serikali inakuja kufuatia Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Hangwa Enos Hangwa, kubainisha changamoto mbalimbali zinazoikumba taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja na uhaba wa watumishi, uchakavu wa miundombinu, na upungufu wa vifaa vya kufundishia kama vile kompyuta na midoli ya kufundishia.

Dkt. Hangwa amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1974, kimefanikiwa kutoa wahitimu 2,255, huku 84 kati yao wakihitimu mwaka huu.

Aidha, ameeleza kuwa chuo kimepanga kuongeza programu mpya tatu katika fani za tiba lishe, mionzi, tabibu meno, na tiba kwa vitendo ikiwa zinalenga kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 270 wa sasa hadi 960.

Malengo yetu ni kuongeza programu hizi ili kupandisha udahili wa wanafunzi na kuboresha kiwango cha elimu chuoni hapa. Hata hivyo, tunaomba Wizara itusaidie kupata fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu na kuharakisha ujenzi wa jengo la kitaaluma,” amesema Dkt. Hangwa.

Ukarabati huu unatarajiwa kuimarisha uwezo wa chuo hicho katika kutoa elimu bora na kuongeza mchango wake katika sekta ya afya nchini.

http://SERIKALI YATENGA BILIONI 2.9 UKARABATI WA CHUO CHA MAAFISA TABIBU MASWA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here