Home LOCAL SERIKALI YAJIZATITI KUHAKIKISHA HAKI ZA WATU WENYE ULEMAVU ZINAZINGATIWA

SERIKALI YAJIZATITI KUHAKIKISHA HAKI ZA WATU WENYE ULEMAVU ZINAZINGATIWA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vyovyote vya unyanyasaji dhidi ya watu wenye ulemavu, akiahidi kuchukua hatua kali kwa wale watakaobainika kuhusika.

Dkt. Biteko alitoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam, alipomwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, katika maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani. Hafla hiyo pia ilihusisha uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi wa Watu Wenye Ualbino na Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi kwa Watu Wenye Ulemavu.

“Serikali imejipanga kupambana na vitendo vya unyanyasaji, ikiwemo mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi. Tunataka kuhakikisha kila mwananchi anaishi kwa heshima na usalama,” alisema Dkt. Biteko huku akiweka msisitizo kwenye hatua za kisheria. 

Kauli mbiu ya mwaka huu, “Kukuza Uongozi kwa Watu Wenye Ulemavu kwa Ajili ya Mustakabali Jumuishi na Endelevu,” inahamasisha uongozi wa watu wenye ulemavu kama njia ya kufanikisha maendeleo jumuishi. Dkt. Biteko alisisitiza kuwa Serikali imeweka miongozo madhubuti, ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwa makundi maalum, ili kuhakikisha utekelezaji wa haki zao unafanyika kwa vitendo.

“Hatuwezi kuruhusu maazimio ya kazi kubaki makaratasi bila utekelezaji. Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu kihakikishe kinafuatilia utekelezaji wa bajeti na mipango katika ngazi za halmashauri,” aliongeza. 

Dkt. Biteko pia aliwataka Wakuu wa Mikoa kuhakikisha halmashauri zinatenga bajeti ya vifaa saidizi kulingana na viwango vya ubora vinavyotakiwa. Aidha, aliagiza Wizara na taasisi zote za kiserikali kutekeleza Mpango Kazi huo kwa mujibu wa maelekezo ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwan Kikwete, alisema Serikali inaendelea kutoa elimu ya haki za kijamii kwa watu wenye ulemavu ili kuimarisha usawa katika jamii.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mhe. Riziki Lulida, alitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika maendeleo ya taifa. “Katika kipindi cha miaka minne, tumeshuhudia mabadiliko makubwa, ikiwemo kushirikishwa kwa walemavu katika sekta za nishati na madini,” alisema Mhe. Lulida.

Mkurugenzi Mtendaji wa HelpAge Tanzania, Smart Daniel, alikumbusha kuwa ulemavu unaweza kumpata mtu yeyote kwa sababu za kuzaliwa, ajali, au uzee, akihimiza umuhimu wa teknolojia saidizi kwa kila mtu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here