Home LOCAL SERIKALI, NMB KUSHIRIKIANA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA

SERIKALI, NMB KUSHIRIKIANA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA

   

Na WAF – Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za afya ikiwemo Benki ya NMB ambapo imeahidi kuchangia Shilingi Bilioni moja kwa ajili ya matibabu kwa watoto wenye tatizo la moyo nchini.

Hayo yamezungumzwa leo Novemba 1, 2024 wakati wa kikao baina ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama na uongozi kutoka Benki ya NMB wakiongozwa na Mkuu wa Idara ya Huduma za Benki kwa Serikali na Msimamizi wa Ofisi ya Makao Makuu Dodoma Bi. Vicky Bishubo kilichofanyika katika ofisi za Wizara ya Afya jijini Dodoma.

Waziri Mhagama ameuomba uongozi wa benki hiyo kuendelea kusaidia kuimarisha mifumo ya mawasiliano katika sekta ya afya, kusaidia Bima ya Afya kwa Wote hususan kaya masikini, uimarishaji wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii pamoja na ujenzi wa wodi maalumu za uangalizi kwa watoto wachanga wagonjwa (NICU).

“Kwakweli tunawashukuru sana kwa kuendelea kuisaidia sekta ya afya, mmekuwa ni miongoni mwa wadau wetu wakubwa, lakini pia tunaomba muendelee kusaidia katika kuimarisha mifumo ya mawasiliano katika sekta ya afya ili taarifa zetu ziwe zinasomana kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa, ujenzi wa wodi maalumu za uangalizi kwa watoto wachanga wagonjwa (NICU) ili kuokoa maisha ya watoto wetu,” amesema Waziri Mhagama.

Benki ya NMB imekua ni mdau mkubwa katika sekta ya afya kwa kusaidia maeneo mengi ikiwemo vitanda vya kujifungulia kwa wajawazito katika hospitali mbalimbali nchini, mashuka, kukarabati majengo ikiwemo ukarabati mkubwa wa wodi ya watoto katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Vilevile, benki hiyo inatoa huduma za kibenki katika vituo vya afya ili kurahisisha upatikanaji na uwekaji wa fedha ambapo ni miongoni mwa uboreshaji wa huduma za afya nchini.

Previous articleMAANA YA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN KUIFUNGUA NCHI.
Next articleDkt. NCHIMBI ATOA HESHMA ZA MWISHO KWA MWILI WA GENERALI MUSUGURI JIJINI DAR
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here