Home BUSINESS NHC KULETA MAGEUZI MAKUBWA YA KIUCHUMI MKOANI LINDI KUPITIA RADI WAKE WA...

NHC KULETA MAGEUZI MAKUBWA YA KIUCHUMI MKOANI LINDI KUPITIA RADI WAKE WA MTANDA COMLEX

NA MWANDISHI WETU,LINDI

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kuwa chachu ya maendeleo katika Mkoa wa Lindi kwa kutoa huduma bora za makazi na biashara kupitia mradi wa kisasa wa Mtanda Complex pamoja na maboresho ya majengo yake katika mkoa huo.

Mradi wa Mtanda Complex, ulioanza ujenzi kwa kujenga maduka na ofisi kwa taasisi za kifedha, umekuwa chanzo cha fursa za kiuchumi na ajira kwa wakazi wa Lindi. Aidha, maboresho ya majengo ya NHC yamelenga kuboresha mazingira ya biashara na makazi kwa wapangaji wake katika mkoa huo.

NHC yajenga fursa za kibiashara kwa wakazi wa Lindi

Kwa mujibu wa Bw.Omari Makalamangi, Meneja wa NHC Mkoa wa Lindi, mradi wa Mtanda Complex umefungua milango kwa wazabuni na wasambazaji wa vifaa vya ujenzi, huku ukitoa ajira kwa zaidi ya vibarua 100. Mradi huu ulioanza rasmi Julai 7, 2024, unaendelea katika hatua ya awali ya uchimbaji wa msingi, uwekaji wa nondo za zege, na kumwaga zege. “Mradi huu uko katika hatua za mwanzo za ujenzi, ambapo kazi zinaendelea kwa kasi ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati,” alieleza Bw. Makalamangi wakati akizungumza hivi karibuni na Maisha ni Nyumba.

Mradi huu unakadiriwa kugharimu Sh. Bilioni 4.2 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 31, 2025. Kulingana na Bw. Makalamangi, mradi wa Mtanda Complex unatoa nafasi za biashara kwa wakazi wa Lindi na kuongeza kipato kwa wajasiriamali wadogo kama mama lishe na baba lishe wanaowahudumia wafanyakazi wa mradi.

Mafundi wakiendelea na kazi za ujenzi wa jengo la kisasa la kibiashara la Mtanda Complex linalojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mkoa wa Lindi

Manufaa kwa Wazabuni wa Vifaa vya Ujenzi

Askari kutoka kampuni ya ulinzi mkoani Lindi (ambaye jina lake halipatikana) akilinda vifaa vya ujenzi katika eneo la mradi wa Mtanda Complex ambao umetoa ajira kwa wakazi wengi wa mkoa huo yakiwemo makampuni ya ulinzi

 

NHC imetoa fursa kwa makampuni mbalimbali katika Mkoa wa Lindi kushiriki kwenye mradi huu kupitia usambazaji wa vifaa vya ujenzi. Miongoni mwa makampuni yaliyonufaika na mradi huu ni Lindi World Distributor na AG Autos, ambayo yamesambaza vifaa kama saruji, nondo, na mchanga kwa ajili ya ujenzi wa msingi. Ushirikiano huu ni sehemu ya mikakati ya NHC ya kuwawezesha wazabuni wa ndani na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa huu.

Mashine ikihamisha udongo katika eneo la ujenzi wa Mradi wa Mtanda Complex 

 

“Mafanikio ya mradi huu yanadhihirisha juhudi za NHC za kuwahusisha wazabuni wa ndani katika miradi yake. Ushirikiano huu unasaidia kuimarisha uchumi wa ndani na kuwapatia fursa za kujiongezea kipato,” anasema Bw. Makalamangi.

Maboresho ya Majengo ya NHC Lindi

Majengo ya NHC Mkoa wa Lindi

Pamoja na mradi wa Mtanda Complex, NHC imefanya maboresho makubwa kwenye majengo yake katika Mkoa wa Lindi, ili kuboresha mazingira ya biashara na makazi kwa wapangaji wake. Kwa sasa, majengo 12 kati ya 16 ya NHC yamekamilika kuboreshwa, huku majengo manne yaliyosalia yakiwa yanaendelea kufanyiwa ukarabati. Maboresho haya yanalenga kuboresha mandhari ya mji na kuvutia wawekezaji zaidi katika mkoa wa Lindi.

Bw. Makalamangi anasisitiza kuwa maboresho haya yanaendana na dhamira ya NHC ya kuhakikisha kuwa huduma bora za makazi na biashara zinapatikana kwa wapangaji wake. “NHC inalenga kutoa huduma za hali ya juu kwa wapangaji wake na kuhakikisha kwamba mazingira ya biashara na makazi yanakidhi viwango vya kisasa,” alisema.

Maendeleo ya NHC katika Mkoa wa Lindi

Kupitia mradi wa Mtanda Complex na maboresho ya majengo yake, NHC inachangia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi ya Mkoa wa Lindi. Mradi huu ni sehemu ya mpango mpana wa NHC wa kupanua uwekezaji katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na kuongeza nafasi za ajira na biashara. Aidha, NHC inachangia kukuza sekta ya huduma za kifedha na biashara katika mkoa huo, na hivyo kusaidia wakazi wa Lindi kufikia huduma bora karibu nao.

Kwa juhudi hizi, Shirika la Nyumba la Taifa limeendelea kuwa mshirika muhimu katika maendeleo ya Lindi, likileta mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa mkoa huo kupitia miradi yake ya kisasa na yenye manufaa kwa jamii.

Previous articleEWURA YAWAKUTANISHA WADAU MOROGORO KUTOA MAONI NA MALALAMIKO YAO
Next articleWAZIRI MKUU MGENI RASMI MKUTANO WA PAMOJA WA MAWAZIRI NA VIONGOZI WA WHO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here