Home LOCAL BASHUNGWA AKABIDHI WAKANDARASI UJENZI MADARAJA MANNE – USHETU, BILIONI 18 KUTUMIKA.

BASHUNGWA AKABIDHI WAKANDARASI UJENZI MADARAJA MANNE – USHETU, BILIONI 18 KUTUMIKA.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametambulisha na kuwakabidhi Wakandarasi Wazawa kutoka Kampuni ya Salum Motors na Jonta Investment kwa Wananchi watakaoanza ujenzi wa madaraja makubwa manne ya Ubagwe, Kasenga, Ng’hwande na Mwabomba yaliyoathiriwa na mvua za El Nino katika Halmashauri ya Ushetu yatakayogharimu Shilingi Bilioni 18.05.

Aidha, Bashungwa ameuagiza Wakala ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga kuwasimamia Wakandarasi hao ili ujenzi wa madaraja hayo ukamilike kwa wakati na viwango vya ubora ili yaweze kutumika katika vipindi vyote.

Hafla hiyo ya kuwakabidhi Wakandarasi imefanyika leo Novemba 30, 2024 katika kijiji cha Bugomba A, Kata ya Ulewe katika Halmashauri ya ushetu Mkoani Shinyanga ambapo Bashugwa ameeleza kuwa ujenzi wa madaraja hayo ukikamilika utaondoa changamoto na adha ya wananchi waliyokuwa wakiipata ya kukatika kwa mawasiliano ya barabara misimu ya mvua kila mara.

Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuelekeza na kutupa fedha hizi ili kujenga madaraja yenye ubora na viwango ili miaka ya mbeleni tutakapokuja kujenga lami katika maeneo hayo, madaraja haya haya yatakuwa na ubora wa kuweza kubeba lami hiyo”, amesisitiza Bashungwa.

Kadhalika, Bashungwa ametoa wiki moja kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Geita kumkabidhi Mkandarasi eneo la mradi wa ujenzi wa daraja la Mwabomba (mita 50) ambalo linaunganisha Halmashauri ya Ushetu na Mkoa wa Geita.

Vilevile, Bashungwa amebainisha kuwa tayari Wizara ya Ujenzi imeipandisha hadhi barabara ya Masumbwe – Mwambomba- Bugomba A – Igombe River (Km 124) kutoka Wilaya na kuwa ya Mkoa ili iweze kuhudumiwa na TANROADS na hivyo kufanya fedha za matengenezo ya barabara katika Jimbo la Ushetu kuongezeka kutoka Bilioni 1.5 kwa mwaka wa fedha 2023/24 hadi kufikia Bilioni 2.7 kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amewataka wananchi kuwa walinzi wa vifaa vya ujenzi pindi miradi hiyo inapotekelezwa kwa kutojihusisha na wizi wa mafuta, nondo na saruji na kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pindi watakapoona uhujumu wowote wa vifaa vya ujenzi.

Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Lutengano Mwandambo ameeleza ujenzi wa Daraja la Ubagwe (m 40) unagharimu Bilioni 4.14, Daraja la Kasenga (m 60) unagharimu Bilioni 5.13, Daraja la Ng’hwande (m 40) unagharimu billion 4.28 na Daraja la Mwabomba (m 50) unagharimu Bilioni 4.5 pamoja na ujenzi wa tuta la barabara (m 300) kwa kiwango cha changarawe katika kila daraja kwa muda wa mwaka mmoja (miezi 12).

Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kuwezesha utekelezaji wa madaraja hayo makubwa ambayo yalipata madhara makubwa na kusababisha wananchi kukosa mawasiliano ya barabara na kukwamisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa wananchi na mazao.

http://BASHUNGWA AKABIDHI WAKANDARASI UJENZI MADARAJA MANNE – USHETU, BILIONI 18 KUTUMIKA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here