Watu takriban 40 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel mashariki mwa Lebanon siku ya Jumatano, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Lebanon.
Afisa wa Israel alisema mashambulizi hayo, yaliyofanyika katika majimbo ya Baalbek na Bekaa, yalilenga wapiganaji wa kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.
Waziri wa Utamaduni wa Lebanon ameeleza kuwa moja ya mashambulizi hayo pia liliharibu vibaya jengo la zamani la enzi za Ottoman karibu na magofu ya Warumi katika Mji wa Baalbek, ambao ni eneo la Urithi wa Dunia la Unesco.
Mashambulizi ya Israel pia yalilenga kusini mwa Beirut siku ya Jumatano, baada ya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) kutoa tahadhari za wananchi kuhama. Jeshi lilisema lilishambulia vituo vya amri vya Hezbollah, maghala ya silaha, na miundombinu mbalimbali iliyopo.
Tahadhari ya baadaye ya IDF ilihusisha vitongoji vinne kusini mwa Beirut, pamoja na eneo karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Lebanon, ambao umeendelea kufanya kazi licha ya mashambulizi ya anga ya Israel kwenye mji mkuu.
Wakati huo huo, kombora lililorushwa na wapiganaji wa Hezbollah kutoka Lebanon liliua mwanaume mmoja karibu na Kibbutz huko Kaskazini mwa Israel, kwa mujibu wa wahudumu wa dharula.