Home BUSINESS WMA YAWAHIMIZA WADAU SEKTA YA MADINI KUTUMIA MIZANI ILIYO SAHIHI

WMA YAWAHIMIZA WADAU SEKTA YA MADINI KUTUMIA MIZANI ILIYO SAHIHI

Na: Mwandishi wetu, GEITA 

Kaimu Meneja Wakala wa Vipimo Mkoa wa Geita, Eva Ikula, amewahimiza wadau katika sekta ya madini kuhakikisha wanatumia mizani iliyohakikiwa na WMA ili kutambua uzito halisi wa madini yanayonunuliwa na kuuzwa.

Ameyasema hayo kwenye maonesho ya saba ya kimataifa ya madini yanayofanyika Mkoani Geita katika viwanja vya EPZA bombambili ambapo WMA inashiriki kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo sahihi katika sekta ya madini na nyinginezo.

“Jukumu la WMA katika sekta hii ni kuhakikisha mizani yote inayotumika kuuzia na kununulia vito na madini inahakikiwa na inapima madini kwa usahihi, lakini pia kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wadau wa Sekta hii” Amesema Eva

Kadhalika, ameeleza kuwa mara baada ya uhakiki wa mizani hiyo kukamilika huwekwa alama maalumu ambayo huonyesha utambuzi kuwa mizani imehakikiwa na inafaa kutumika katika biashara mbalimbali za madini.

“Alama zinazowekwa katika mizani iliyohakikiwa ni stika pamoja na lakiri (seal) ambayo inakuwa na alama ya nembo ya taifa pamoja na tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika mfano 24 ikiashiria imehakikiwa 2024” Ameongeza Eva.

Akifafanua zaidi amesema kuwa pamoja na majukumu mengine ya Wakala katika kuhakiki mizani hiyo,WMA imekuwa ikifanya kaguzi za kushitukiza katika maeneo mbalimbali ya biashara za madini ili kubaini usahihi wa matumizi ya mizani hiyo.

“kaguzi zetu hufanywa kushitukiza katika masoko kumi yaliyopo hapa kwetu geita ambayo ni Geita mjini, Katoro, Chato, Lwamgasa, Nyarugusu, Mbogwe, Bukombe, Nyang’wale, Mgusu na Nyakagwe, lakini pia na masoko mengine nchini kote” amesema 

Kwa upande wake Patrick Charles, mfanyabiashara katika soko kuu la dhahabu Geita, ameishukuru Serikali kupitia kwa wakala wake WMA kwa kuendelea kusimamia sekta ya madini nchini.

“Wito wangu kwa wafanyabiashara wenzangu hapa sokoni tuhakikishe mizani yetu imekaguliwa na Wakala wa serikali WMA hii ni faida kwetu kwani kwa kupitia vipimo sahihi ndio tunaweza kupata haki yetu kama wauzaji na hata wale tunaowauzia, haya ni matakwa ya sheria ya vipimo”. Amesema Patrick

Wakala wa vipimo imekuwa ikishiriki maonesho haya tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018, huku ikijikita katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini, maji, umeme, gesi, mazao na nyinginezo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here