Home BUSINESS WAZIRI CHANA AELEKEZA HALMASHAURI KUDHIBITI MATUKIO YA MOTO MISITUNI

WAZIRI CHANA AELEKEZA HALMASHAURI KUDHIBITI MATUKIO YA MOTO MISITUNI

 Na; Happiness Shayo – Makete

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amezielekeza Halmashauri zote nchini kuzuia mianya inayosababisha moto kwenye maeneo ya misitu huku akisisitiza matumizi ya Sheria ndogo za Misitu.

Ameyasema hayo leo Oktoba 8, 2024 katika kikao kilichofanyika Halmashauri ya Wilaya ya Makete Mkoani Njombe.

“Kila kikao cha Serikali ya kijiji ajenda ya kudhibiti moto iwe ya kudumu na ninashauri kamati ya kudhibiti matukio ya uchomaji moto iwe mpaka kwenye ngazi ya kijiji au kata” amesisitiza Mhe. Chana.

Aidha, amesisitiza kuhusu kufanya ulinzi shirikishi ili kujua waanzilishi wa moto sambamba na kufanya tafiti za miti inayofaa kwa mkaa ili wananchi wapewe vibali vya kuipanda waachane na uchomaji misitu.

Awali, akiwasilisha taarifa ya matukio ya uchomaji moto ovyo Wilayani Makete kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2024/2025, Afisa Misitu, George Africanus alisema kuwa jumla ya eneo lenye ukubwa wa ekari 1960 zimeungua kwa moto zenye thamani ya shilingi bilioni 1.4.

Amefafanua kuwa moto huo ulitokea katika kata za Mbalatse, Mang’oto na Matamba ambapo moto huo umeunguza miti ya kupandwa, miti ya asili, mashamba na nyasi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Makete,Juma Samwel Sweda amesema Halmashauri inaendelea na zoezi la kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuacha kuchoma misitu na kuunda Kamati za kudhibiti moto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here