Na Mwandishi Wetu,Chalinze
WAUGUZI 200 katika Halmashauri ya Wilaya Chalinze Mkoani Pwani ambao wanaohudumia wamama wenye watoto njiti wamepatiwa mitungi ya gesi ya Oryx 200 pamoja na majiko yake kwa lengo la kuwawazesha kutumia muda mwingi kuwahudumia wamama hao badala ya kuhangaika kutafuta kuni na mkaa.
Mitungi hiyo imetolewa na Kampuni ya Gesi ya Oryx kwa kushirikiana na Doris Mollel Foundation ambapo wauguzi hao wametakiwa kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa mama wenye watoto njiti pamoja na wagonjwa wengine wanaowahudumia wodini.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi hiyo kwa wauguzi hao iliyofanyika katika Hospitali ya Msoga,Mbunge wa Jimbo la Chalinze na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana,Ajira na Watu Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amesema wanatambua mchango Mkubwa wa Oryx na Dorris Mollel Foundation katika kumuunga mkono Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia na kutoa mitungi kwa wauguzi hao kuna tija kubwa.
“Wauguzi Wetu kupatiwa mitungi hii ya gesi Moja ya faida ambayo inakwenda kupatikana sasa watakuwa na muda wa kutosha kuhudumia mama wenye watoto njiti katika hospitali yetu, kuni na mkaa unasababisha muda mwingi kupotea lakini kutumia gesi muda ni muda Mdogo tu.
“Hata hivyo oryx na Doris Mollel Foundation mnaweza kuona kama mnaunga mkono juhudi za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia lakini kwa namna
moja au nyingine mnatusaidia sana katika kulinda mazingira yetu kwani watu sasa hawataingia maporini,” amesema Ridhiwani.
Akieleza zaidi kupitia mitungi ya gesi iliyotolewa kwa wauguzi sasa watu wanakwenda kuwa salama lakini kazi iliyobakia kwao na Mkurugenzi ni kuhakikisha wanahamasisha watu kutumia nishati safi ya kupikia kwani kumekuwa na ukataji mkubwa wa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa.
“Mtakuwa mashuhuda mkaa uliokuwa unapelekwa Dar Salaaam katika kipindi cha miaka mitatu hadi minne iliyopita zaidi ya asilimia 88 inatoka Chalinze, tulilazimika kufanya operesheni maalum kuangalia huko ndani ya Hifadhi ya Wamimbiki mambo yanavyokwenda, ukipita nje unaonekana msitu mkubwa lakini ukiingia ndani hakuna miti
“Hivyo halmashauri yetu kwa kushirikiana na wadau wakiwemo wenzetu wa hifadhi ya Wami Mbiki wamefanya kazi kubwa ya kuhakikisha mazingira tunaweka vizuri.Niwashukuru Oryx ninyi ni wadau namba moja wa nishati safi Chalinze,”amesema na kuendelea kuwapongeza kwa jitihada wanazofanya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake Evarist Kisaka ambaye ni Mwakilishi wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania amesema wamefika hospitali ya Msoga kwa ajili ya kupatiwa mitungi 200 ya gesi ya Oryx wauguzi wanaohudumia mama wenye Watoto Njiti ili kuhakikisha wanapata muda mwingi kuhudumia watoto hao badala ya kuhangaika kutafuta kuni na
Mkaa.
“Tunajua kutumia kuni na mkaa kunapoteza muda mwingi kutafuta kuni lakini muda mwingi unapotea katika kuwasha moto, hivyo Oryx kwa kushirikiana na Doris Mollel Foundation tumeona iko haja ya kuwpatia mitungi ya gesi wauguzi hawa ili wapate muda wa kutosha kuwahudumia Watoto Njiti .Pia kuwapatia mitungi hii ni kulinda afya za wauguzi wetu ili waendelee kuwahudumia vizuri akina mama wenye watoto njiti na ukiachana na hayo tunahakikisha tunalinda mazingira kwa ujumla.
“Mitungi 200 ambayo tumeigawa leo tunaamini tunakwenda kuwasaidia kwa kiasi kikubwa wauguzi hawa kwani kutumia gesi gharama ziko chini ukilinganisha na kutumia kuni au mkaa.Gunia la mkaa la Sh.80000 kwa familia ya watu watatu linatumika ndani ya mwezi mmoja wakati akitumia gesi atatumia gharama za chini ambazo hazitazidi 50,000.”
Kwa upande wake Alice Mwakatika ambaye ni Msimamizi wa miradi kutoka Dorris Mollel Foundation amesema kwa kushirikiana na Oryx wamegawa mitungi 200 kwa wauguzi na malengo ya kugawa mitungi hiyo ni katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo ni kampeni mahususi ya kidunia na Afrika imepewa nguvu na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan .
“Tumewapa mitungi wauguzi hawa kwakuwa tunajua wanakuwa na muda mwingi na wagonjwa hasa wamama kwasababu sisi tumejikita katika afya ya uzazi mama na mtoto, tunajua katika hawa wauguzi wako wakunga na wapo wanaokaa na watoto wodini kwahiyo hawa tukianza kuwaelimisha watakuwa mabalozi wa nishati safi na watapeleka elimu hiyo kwa wamama wajawazito na wagonjwa wengine ambao ndio muda mwingi wanakaa nao wodini.”
Aidha ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuunga mkono kampeni ya nishati safi ya kupikia ambayo ni ajenda ya dunia nzima na kwa Tanzania kampeni hiyo imepewa msukumo mkubwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa kinara wa nishati safi ya kupikia, hivyo anastahili kuungwa mkono na Watanzania.
Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Gabriela Mtwale amesema wanashukuru kwa kupatiwa mitungi 200 ya gesi ambayo imetolewa na Oryx na kwamba watahakikisha wanahamasisha wauguzi kutumia nishati safi kwani hata Rais Samia anahimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia kwasabababu kutumia kuni au kuna athari nyingi za kiafya lakini kimazingira.
Mwisho.