Home BUSINESS VYAMA VYA USHIRIKA BADILIKENI

VYAMA VYA USHIRIKA BADILIKENI

Serikali imeendelea kutoa msisitizo kwa Vyama vya Ushirika na kuvitaka kujenga misingi imara ya ushirika ili kumlinda mkulima badala ya kumnyonya na kumdhulumu haki zake.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) tarehe 1 Oktoba 2024 wakati akizindua Kiwanda cha Kubangua Korosho cha TANECU kilichopo Newala, Mkoani Mtwara.

Waziri Bashe amesema safari ya kuvikwamua vyama vya ushirika haikuwa rahisi kwa kuwa vilikuwa na madeni ya zaidi ya shilingi bilioni 17 na benki zilikuwa zinawakwepa kuwakopesha. “Kujenga ushirika imara ndiyo msingi wa kumsaidia mkulima mdogo. Leo tasnia ya korosho ina taswira tofauti na sasa tunajadili kiwanda cha TANECU cha kubangua korosho,” amesema Waziri Bashe.

Aidha, Waziri Bashe amekipongeza Chama Kikuu cha Ushirika cha TANECU Ltd. kwa kuwa mfano mzuri wa kuonesha ushirika unaozidi kuwa imara kwa kuhakikisha uwekezaji huo wa kiwanda ni wa wakulima wenyewe. “Naelekeza pia kijengwe kiwanda kingine kama hiki kule Tandahimba ili kiwe tayari wakati wa msimu wa mwaka ujao,” amesema Waziri Bashe.

Kiwanda cha TANECU kimegharimu shilingi bilioni 3.4 na kina uwezo wa kubangua tani 3,500 kwa mwaka. Mkakati ni kuwa na viwanda 20 vya Kubangua Korosho chini ya TANECU katika Mkoa wa Mtwara ambapo 10 vitajengwa Newala (tayari 1 kimezinduliwa); na 10 vitajengwa Tandahimba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here