Home LOCAL VIONGOZI,WAUMINI NA WANANCHI WAUNGANA KATIKA KUMBUKIZI HAYATI BABA WA TAIFA

VIONGOZI,WAUMINI NA WANANCHI WAUNGANA KATIKA KUMBUKIZI HAYATI BABA WA TAIFA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na Mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wameungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi,waumini na wananchi mbalimbali katika Ibada ya Misa Takatifu ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu. Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Francis Xavier iliyopo Nyakahoja Jijini Mwanza.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mara baada ya kumalizika kwa ibada hiyo, Makamu wa Rais amesema serikali inawashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuliombea Taifa pamoja na Viongozi wake.

Makamu wa Rais amesema Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ameacha misingi imara inayojenga Taifa imara ambayo viongozi wa sasa na wajao hawana budi kuiendeleza.
Ametaja mambo mbalimbali ambayo Baba wa Taifa alitekeleza enzi za uhai wake kama ifuatavyo.

✓ Aliongoza kwa ustadi jitihada za kuipatia Tanganyika uhuru na kuunganisha makabila zaidi ya 120 na kuwezesha kutumika kwa lugha moja ya kiswahili. Alibainisha wazi wazi nia yake ya kuchelewesha uhuru wa Tanganyika hadi nchi nyingine ziwe huru. Chini ya uongozi wake, Tanzania ilitoa rasilimali zake kusaidia harakati za ukombozi wa nchi nyingine, Mf. Msumbiji, Angola, Namibia, Afrika Kusini.
✓ Alikuwa Mwanamajui (Pan-Africanist) halisi, aliyeasisi muungano wa Tanganyika na Zanzibar na alikuwa miongoni mwa waasisi wa Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU) kwa lengo la kuwaunganisha Waafrika.
✓ Mwalimu alikuwa mpenda amani. Ametuachia tunu ya amani na kuifanya nchi yetu kuwa kisiwa cha amani. Aidha, alikuwa msuluhishi mahiri wa migogoro ya Mataifa mengi Barani Afrika, mf. Burundi.

✓ Alisimamia ulinzi wa Taifa letu kwa nguvu zote. Kwa mfano, Nduli Idd Amini alipojaribu kukalia kipande cha ardhi yetu, Mwalimu aliwaongoza Watanzania kumfukuza mvamizi huyo na kuwasaidia Waganda kumwondosha kabisa.
✓ Alithamini sana haki ya kupata elimu kwa maendeleo ya Taifa na alitoa mchango mkubwa kupitia taaluma yake ya ualimu na pia Serikali yake iligharamia Watanzania kusoma ndani na nje ya nchi katika fani mbalimbali kama ulinzi, afya, uchumi, maji, kilimo ili kupata wataalam wa kutosha.
✓ Alikuwa kiongozi mzalendo kweli kweli, ambaye hakujilimbikizia mali bali alijitoa ili kutatua changamoto za wananchi wake. Aliasisi maadili ya Viongozi wa umma na kuyaishi, pamoja na kupiga vita rushwa kwa maneno na vitendo.
✓ Katika kujenga na kuimarisha uzalendo miongoni mwa vijana na kujitoa kwa moyo kulitumikia Taifa lao pasipo kuchoka, Mwalimu alianzisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

✓ Alihimiza kilimo kwa vitendo, akifundisha kuzingatia kanuni bora za kilimo kama matumizi ya pembejeo, mbegu bora n.k.
✓ Alikuwa mtunzaji na mhifadhi mahiri wa mazingira. Alianzisha na kutunza msitu wa miti ya asili Kijijini kwake Mwitongo – Butiama.
✓ Alimtegemea sana Mungu na alikuwa mwenye bidii ya kusali wakati wote.
Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza katika kujiandikisha kwaajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa. Amewasihi wenye uwezo kujitokeza katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.


Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
14 Oktoba 2024
Mwanza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here