Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, inaonekana kupendelewa zaidi na China katika kanda ya Afrika Mashariki, huku mataifa hayo yakishirikiana katika maendeleo ya miundo mbinu, ikiwa ni Pamoja na ujenzi wa kambi ya kijeshi ya China katika pwani ya Bahari Hindi.
Balozi wa China nchini Tanzania Cheng Mingjian, hivi karibuni alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kijeshi na Tanzania, katika kuboresha uhusiano wa pande hizo mbili, hatua inayoashiria ukuaji wa urafiki kati ya nchi hizo mbili.
Akiwa katika mwaka wake wa tatu afisni, balozi huyo wa Jamuhuri ya watu wa China nchini Tanzania, ametekeleza jukumu la msingi la kuimarisha uhusiano ambao matokeo yake ni bayana katika sekta zingine za maendeleo.
Ushirikiano huo muhimu kati ya China na Tanzania umedumu tangu aliyekuwa makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, alipochukua hatamu za uongozi mwezi Machi mwaka 2021, baada ya kifo cha John Pombe Magufuli akiwa madarakani.
Chini ya himaya ya Suluhu, iliyowiana na muhula wa Cheng’ ulioanza mwezi Disemba mwaka 2021, nchini hizo mbili zimepiga hatua kubwa katika ushirikiano wa kibiashara, huku China ikiwa chanzo kikuu cha uwekezaji wa kigeni.
Miongoni mwa ushirikiano wa pande hizo mbili ni pamoja na miradi ya miundo msingi kama vile ujenzi wa mabarabara, reli ya kisasa ya SGR na bandari, ambazo ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya uchukuzi nchini Tanzania.
China pia imehusika katika kupiga jeki sekta ya elimu nchini humo, kwa kuwafadhili wanafunzi raia wa Tanzania kuendeleza masomo yao jijini Beijing, pamoja na kufadhili mipango ya kubuni soko la utamaduni wa China nchini Tanzania.
Wachanganuzi wa maswala ya kimataifa wamedokeza kuwa uhusiano mzuri unaoshuhudiwa kati ya Rais Suluhu na balozi Cheng, umechochea ushirikiano wa kupigiwa mfano kati ya nchi hizo mbili.
Ikizingatiwa kuwa balozi Cheng awali alihudumu wadhifa wa naibu Mkurugenzi Mkuu wa idara ya usalama wa nje katika wizara ya China ya Mambo ya Nje (MFA) jijini Beijing, hatua hiyo inampa fursa bora kufanikisha miradi ya maendeleo nchini anzania.
Ufanisi wake mkuu umetajwa kuwezesha kuafikiwa makubaliano na Tanzania kwa ujenzi wa kambi ya kijeshi jijini Dar-es-Salaam, na kuifanya kuwa kituo kikubwa zaidi cha jeshi la China barani Afrika.
Wachanganuzi wa maswala ya kisiasa katika kanda ya Afrika Mashariki, wanadokeza kuwa, Rais Suluhu huenda hajapiga hatua kubwa kisiasa ikilinganishwa na alivyofanya mtangulizi wake, lakini amevutia zaidi maendeleo ya miundo msingi, kutokana sera yake ya kuegemea taifa hilo la mashariki.
Huenda swala hilo halimo wazi kwa kizazi kichanga cha sasa ambacho kina idadi kubwa ya watu, lakini wengi walioishi miaka ya Nyerere wanahisi kuwa masalio ya mfumo wao wa Ujamaa kwa fikra za wachache uongozini, waifanya rahisi kwa Tanzania kuegemea kwa upande wa China barani Afrika.
Tanzania ilikumbatia mfumo wa Ujamaa na kuegemea upande wa Mashariki wakati wa utawala wa zaidi ya miaka 25 ya msomi Mwalimu Julius Nyerere. Miaka mingi baada ya kifo cha Nyerere na hata baada ya kujutia mkondo wa kisiasa aliouchukua, Tanzania ingali imeathiriwa na mfumo wa Ujamaa.
Kulingana na Bradley Ouna, mtaalam wa sheria kutoka chuo kikuu cha Dar-Es-salaam: “Mfumo wa Ujamaa uliwalazimisha raia wa Tanzania kuishi pamoja na kufanya kazi kwa kutegemeana, hatua iliyomaliza ukabila, lakini ulikumbwa na gharama ya juu ya uchumi kutokana na uzalishaji duni wa bidhaa na ukosefu wa ushindani wa kibiashara.
Mwishoni mwa muhula wake wa Urais, Nyerere alikiri kuwa mfumo huo ulifeli, kwa sababu ya changamoto za kifedha. Kulingana naye, Ujamaa ulihitaji ufadhili mkubwa kutoka kwa serikali.
Wakili kutoka Tanzania Mutatina Oswald anasema, “Uwekezaji wa China unaonyesha upande mzuri kama vile kubuni nafasi za ajira kwa raia wa Tanzania katika wilaya ya Kariokor Jijini Dar es Salaam, ambako viwanda vingi vimejengwa. Licha ya kuwa siwezi kusema ni China inaendesha Uchumi, wamechangia pakubwa katika ukuzaji wa teknolojia, miundo mbinu na biashara.
Huku jeshi la China likionekana kuimarisha usalama na kulinda njia za baharini za kibiashara, huenda kukawa na wasiwasi miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki, zinazohisi jeshi la Tanzania linazidi kuimarika kuliko majirani wake.
Mwanadiplomasia, kutoka mataifa ya magharibi, anasema kuwa uwepo wa jeshi la China nchini Tanzania, utasababisha Tanzania kupigiwa kurunzi hasaa na nchi za Magharibi kama vile Marekani, ambazo huwa na wasiwasi na shughuli za China katika mshirika wake wa awali, na kusababisha ushindani wa kimataifa katika taifa hilo la Afrika.
Wataalam wa kidiplomasia wanasema kuwa ni muda tu utabainisha kama uhusiano kati ya nchi hizo mbili utadumu, hususan iwapo Suluhu atashinda Urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Mwandishi ni msomi wa kimataifa ambaye hutoa maoni kuhusu uhusiano wa kidiplomasia.