Yagawa mabomu baridi 2,567 Kwa Kanda 7 kuimarisha zoezi la kufukuza tembo.
Na. Joyce Ndunguru, Morogoro.
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, imegawa mabomu baridi 2,567 kwa Makamanda wa Kanda (7) za Uhifadhi za TAWA kwa ajili ya kuendelea kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Hafla hiyo ya ugawaji wa vifaa imefanyika leo Oktoba 5, 2024, katika Makao Makuu ya TAWA yaliyopo Mkoani Morogoro na kuongozwa na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda.
Akiongea wakati hafla hiyo, Kamishna Mabula amesema TAWA imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti wanyama wakali ikiwemo kuimarisha doria za muitikio wa haraka, kushirikisha askari wa vijiji 184, kujenga vituo vya udhibiti, kununua vitendea kazi ikiwemo magari, ndege nyuki, pikipiki na vilipuzi sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kuepukana na kukabiliana na madhara yaletwayo na wanyamapori wakali.
” Katika mwaka wa 2024-2025, TAWA imepanga kuendelea kujenga vizimba vya kudhibiti mamba, kuchimba mabwawa na kununua ndege nyuki zenye uwezo wa kumwaga maji yenye pilipili kwa ajili ya kufukuza tembo kwenye maeneo ya wananchi”, amesema Kamishna Mabula.
Aidha, Kamishna Mabula amewaelekeza Makamanda kuhakikisha kuwa Askari wa uhifadhi na Askari wa vijiji wanapatiwa mafunzo stahiki ya kutumia mabomu baridi na wahakikishe kuwa mabomu hayatumiwi na wananchi.
Vilevile Kamishna Mabula alitoa rai kwa wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa wahifadhi wa wanyamapori kwa kuzingatia ushauri wanaopewa na wataalamu ikiwemo kuacha kufanya shughuli za kibinadamu maeneo ya shoroba, kuacha matembezi ya usiku yasiyo na lazima na kuchukua tahadhari wanapofanya shughuli za binadamu katika mito, mabwawa na maziwa.
Sambamba na ugawaji wa mabomu baridi hayo, Makamanda wa Kanda za Uhifadhi pia wamekabidhiwa vitendea kazi vingine ikiwemo vuvuzela (548), tochi (1,451) na filimbi (500). Vifaa hivi visivyo na mlipuko vitagawiwa kwa wananchi kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kanda ya Kusini Mashariki, Abraham Jullu, kwa niaba ya Makamanda wa Kanda za Uhifadhi alitoa shukrani kwa kukabidhiwa vitendea kazi hivyo na alisema kuwa vitendea kazi hivyo vitasaidia sana katika kupunguza madhara yatokanayo na mnyamapori tembo.