Home LOCAL TAWA IMEJIZATITI KULINDA MAISHA YA WANANCHI DHIDI YA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU

TAWA IMEJIZATITI KULINDA MAISHA YA WANANCHI DHIDI YA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Kwa umma wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini – TAWA Beatus Maganja amesema taasisi ya TAWA imejipanga vyema katika kulinda maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu nchini.

Maganja ameyasema hayo Oktoba 06, 2024 Katika Kijiji cha Igunguli kilichopo Kata ya Loje wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma alipokuwa akitoa elimu kwa wakazi wa Kijiji hicho hususani wavuvi wanaofanya shughuli zao katika bwana la mtera wakati wa ziara ya kutoa elimu ya kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu.

“Sisi tumedhamiria, tumejizatiti na tumejipanga kwamba tutasimama na wananchi kuhakikisha, kwanza tunawapa elimu, lakini pia kulinda maisha yenu kwa kuendelea kufanya doria za mara kwa mara ili kuhakikisha usalama wenu” amesema Maganja

Akizungumzia hatua ambazo Mamlaka hiyo imekuwa ikichukua katika kukabiliana na changamoto ya mamba na viboko katika bwawa la mtera Maganja amesema TAWA imeimarisha doria zinazoshirikisha Askari wahifadhi na wanyamapori wa vijiji na kutoa elimu kwa jamii ya namna ya kujikinga na kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao.

Kufuatia jitihada hizo Maganja amesema katika kipindi cha kuanzia Januari 2024 mamba watatu (3) na Viboko wawili (2) waliokuwa hatarishi Kwa maisha ya watu na mali zao walidhibitiwa na zaidi ya wananchi 300 wakiwemo wavuvi zaidi ya 40 walipatiwa elimu Katika vijiji vilivyopo Kata ya Migoli.

Aidha Afisa huyo amesema katika kuimarisha ulinzi ya watu wanaoishi Kando ya Bwawa la Mtera , Mamlaka imeanzisha kituo cha kudumu cha Askari Katika Kijiji cha Igunguli na Kijiji cha Migoli, kituo chenye jumla ya Askari 20 ambao wamepatiwa vitendea kazi muhimu Kwa ajili ya udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu.

Katika hatua nyingine Maganja ametoa rai Kwa wananchi kuendelea kufanya shughuli zao kama kawaida isipokuwa wachukue hadhari wanapokuwa kwenye mabwawa, mito na madimbwi.

Vilevile amewasisitiza kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa uhifadhi ikiwemo kuacha kuoga au kufua ndani ya bwawa na wavuvi kutumia nyenzo ZA kisasa katika shughuli za uvuvi huku akiwataka kutoa taarifa kwa haraka Kwa wataalamu wa uhifadhi au Serikali za vijiji husika ili hatua stahiki zichukuliwe Kwa haraka.

Naye Afisa Uelimishaji kutoka TAWA Irene Bonaventure Midala amesema Katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 Serikali imetenga bajeti ya ujenzi wa Kizimba kimoja ambacho kitajengwa Katika Kijiji kimojawapo kati ya vijiji vinavyozunguka bwawa la mtera lengo likiwa ni kupunguza changamoto ya wanyamapori hao.

Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Igunguli wamepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA hususani Kwa elimu wanayoitoa ambayo wanakiri imekuwa msaada kwao lakini pia mwitikio wa haraka pale inapotokea changamoto ya wanyamapori hao.

Previous articleMBUNGE WA BUSANDA AHIMIZA WAJASIRIAMALI KURASIMISHA BIASHARA
Next articleRC CHALAMILA AZINDUA KAMPENI SHELL TUMERUDI KIVINGINE KATA KILOMITA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here