Home LOCAL TARURA YATEKELEZA AGIZO LA RAIS SAMIA UJENZI DARAJA LA MAWE LEBENYA

TARURA YATEKELEZA AGIZO LA RAIS SAMIA UJENZI DARAJA LA MAWE LEBENYA

#Ujenzi wake wafikia 75%

Gairo, Morogoro

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Gairo Mkoa wa Morogoro, imetekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kujenga daraja la mawe la Lebenya lenye urefu wa mita 45 linalounganisha Wilaya za Kilindi, Gairo na Kilosa mkoani Morogoro kutoka kwenye fedha zilizobaki wakati wa ujenzi wa daraja la Berega.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalum ), Mhe. Kapt. George Mkuchika alipofika katika daraja hilo ili kukagua hatua iliyofikia ambapo ujenzi wa daraja hilo umefikia 75% kukamilika.

Mhe. Mkuchika amesema Mhe. Rais Samia ametoa mabilioni ya fedha ili kurejesha mawasiliano kwa wananchi kwa kujenga upya madaraja yaliyoharibiwa na mvua zilizonyesha mwaka jana ambazo ziliathiri miundombinu ya barabara katika maeneo mengi nchini.

Nimefurahi agizo la Rais Samia limetekelezwa, hapa mnajengewa daraja tena mawe tupu, daraja hili litakapokamilika litasaidia shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa hapa”, alisema.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA Wilaya ya Gairo, Mhandisi Simon Masala alisema wametekeleza agizo la Mhe. Rais kwamba, kiasi cha fedha shilingi bilioni 1.3 zilizobaki kwenye ujenzi wa daraja la Berega zitumike kuboresha barabara ya Berega – Kinyolisi – Makuyu Km 18, ujenzi wa daraja la mawe na maboksi kalavati ambapo mpaka sasa ujenzi wa daraja umefikia 75% kukamilika na unatarajiwa kukakamilika tarehe 15/05/2025.

Alisema daraja hilo linagharimu shilingi milioni 373 ambapo kukamilika kwake litanufaisha kata saba zenye jumla ya wakazi 766,507 na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao kwa wakazi wa wilaya ya Gairo, Kilosa na Kilindi.

“Barabara hii ni njia fupi kutoka Kilindi mkoani Tanga kwenda Morogoro ambapo ni Km 18 tu kufika njiapanda ya kwenda Morogoro badala ya kupitia njia ya Gairo ambayo ni Km 44 ambapo ikikamilika itakuza uchumi kwani wananchi watasafirisha mazao yao misimu yote.

Naye, mkazi wa kijiji cha Italagwe-Gairo, Bw. John Semwenda ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo ambapo alisema litakapokamilika watasafirisha mazao yao hususan mbaazi kwenda sokoni kwa urahisi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here