Home INTERNATIONAL TANZANIA YANG’ARA KIMATAIFA KWA KUWA NA KITUO CHA UFUATILIAJI MAJANGA, WADAU WA...

TANZANIA YANG’ARA KIMATAIFA KWA KUWA NA KITUO CHA UFUATILIAJI MAJANGA, WADAU WA MAAFA WAVUTIWA

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akiwasilisha mada kuhusu masuala yua menejimenti ya maafa Tanzania aliposhiriki Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa na Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi (High Level Meeting) kuhusu masuala ya kupunguza athari za maafa vinavyofanyika Windhoek nchini Namibia. Mikutano hiyo inafanyika kuanzia tarehe 21 hadi 24 Oktoba, 2024.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (katikati) pamoja na meza kuu wakifuatilia mada wakati wa vipindi vya kuwasilisha na kujadili namna ya utekelezaji wa masuala ya maafa katika nchi za Afrika aliposhiriki katika Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa Windhoek nchini Namibia.

Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Charles Msangi akiwasilisha mada wakati wa vikao hivyo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akifuatilia mada aliposhiriki Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa vinavyoendelea Windhoek nchini Namibia.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akiteta jambo na Mkurugenzi wa Afrika katika Masuala ya Hali ya Hewa kutoka shirika la hali ya hewa (WMO) Dkt. Agness Kijazi wakati wa Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa vyokilichofanyika Windhoek nchini Namibia.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Ladislaus Chang’a akichangia jambo wakati wa Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa kinachofanyika Windhoek nchini Namibia.

Mkurugenzi wa Afrika katika Masuala ya Hali ya Hewa kutoka shirika la hali ya hewa (WMO) Dkt. Agness Kijazi akiwasilisha mada wakati wa Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa kinachofanyika Windhoek nchini Namibia.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watanzania walioshiriki Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Athari za Maafa na Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi (High Level Meeting) kuhusu masuala ya kupunguza athari za maafa vinavyofanyika Windhoek nchini Namibia. Mikutano hiyo inafanyika kuanzia tarehe 21 hadi 24 Oktoba, 2024.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

 NA. MWANDISHI WETU- WINDHOEK

Tanzania imetajwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kwa kuwa na Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema (National Emergency Operation and Communication Center Situation Room) katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura nchini Tanzania ambacho kimeifanya nchi kuwa kinara katika masuala ya menejimenti ya maafa hususan katika kuzuia, kupunguza kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ametoa kauli hiyo 23 Oktoba, 2024 jijini Windhoek nchini Namibia wakati akiwasilisha mada katika Kikao cha Tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la Kupunguza Madhara ya Maafa na Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi kuhusu masuala ya kupunguza madhara ya maafa.

Akizungumzia umuhimu wa kituo hicho, Dkt. Yonazi amesema kituo hicho kimeendelea kutumika kufanya ufuatiliaji wa uwezekano wa kutokea kwa majanga kwa kutumia mifumo ya kiteknolojia ya kijiografia kwa majanga yanayotokana na hali ya hewa na haidrolojia kwa kutumia jukwaa la kielektroniki la MyDEWETRA.

Mfumo huu umerahisisha ufuatiliaji wa mwenendo wa janga lililotabiriwa na kufanya uchambuzi wa kiwango cha madhara kwa jamii, miundombinu na mazingira, kuandaa taarifa za tahadhari ya mapema ya hatua za kuchukua ili kuzuia, kujiandaa na kukabili maafa, kuandaa taarifa ya mwenendo wa tukio na kusambaza kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kusaidia uratibu na utekelezaji wa shughuli za kukabili na kurejesha hali,” Amesema Dkt. Yonazi

Dkt. Yonazi amesema kuwa uanzishwaji wa kituo hicho cha ufuatiliaji wa majanga na tahadhari ya mapema umefanikiwa kutokana na mradi ulioanzishwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa katika Kanda ya Afrika na kufadhiliwa na Serikali ya Nchi ya Italia kupitia Shirika la Maendeleo la Italia (Italian Agency for Development Cooperation) ambapo Taasisi ya CIMA Research Foundation ya Italia imesadia kutoa utaalam wa utekelezaji wa shughuli zote.

Ameongeza kuwa uwepo wa kituo hicho umesaidia sana Tanzania kuendelea kuwa kinara namba moja katika kukabiliana na maafa kabla hayajaleta madhara.

Kufuatia umuhimu wa kituo hicho, Dkt. Yonazi ametoa wito kwa Nchi wanachama pamoja na mataifa mengine kuja Tanzania kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa kuzingatia umuhimu wake.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoshiriki katika Kikao hicho cha siku nne ambacho kinatajia kumalizika Oktoba 24, 2024 ambapo kikao hicho kimefanikiwa kuwakutanisha wadau zaidi ya elfu moja wa maafa kwa nchi za Afrika wakiwemo wataalamu kutoka katika ngazi za kitaifa, Serikali za mitaa, Mashirika ya Umoja wa Kitaifa na Kimataifa, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti na wanahabari.

Previous articleSERIKALI: KILA HALMASHAURI KUWA NA MSITU WA ASILI KUTUNZA MAZINGIRA
Next articleMAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA MAAFISA WAANDAMIZI WA MAGEREZA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here